Na John Gagarini, Mkuranga
WILAYA ya Mkuranga mkoani Pwani imewasimamishia malipo
watumishi 15 ambao wameondoka kwenye vituo vyao vya kazi bila ya taarifa kwa
mwajiri wake ambaye ni Halmashauri.
Hayo yalisema na mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Abdala Kihato alipokuwa
akisoma taarifa ya wilaya wakati wa ziara ya mkuu wa mkoa wa Pwani kutembelea
shughuli za maendeleo kwenye wilaya hiyo.
Kihato alisema kuwa mishahara hiyo ilizuiliwa kutokana na
watumishi hao kutotoa taarifa walipoondoka kwenye vituo vyao vya kazi wakati wa
uhakiki watumishi katika zoezi la kutambua watumishi hewa.
“Tulifanya uhakiki wa watumishi 179 na kubaini kuwa watumishi
85 walikuwa ni watoro ambapo 51 wamehamia kwenye vituo vingine vya kazi 10
hawakujitokeza na 15 ndiyo walioondoka kwenye vituo vya kazi bila ya taarifa na
watano ni watoro kabisa,” alisema Kihato.
Alisema kuwa zoezi hilo ni endelevu na linaendelea kwani
linaoneka lina changamoto nyingi katika kubainisha watumishi hewa na wale ambao
wako kisheria.
“Hatua tuliyoichukua kwa wale ambao waliondoka kwenye vituo
vyao vya kazi bila ya taarifa ni kusimamisha mishahara yao ili wasije wakwa
wanachukua fedha pasipo kufanya kazi,” alisema Kihato.
Kwa upande wake Ndikilo alisema kuwa maofisa utumishi
wanapaswa kutoa ushirikiano kwa serikali katika kuhakikisha watumishi hewa
wanapatikana na itawachukulia hatua kali wale watakaowaficha watumishi hewa.
Ndikilo alisema kuwa zoezi hilo litakapokamilika mkoa utatoa
taarifa juu ya zoezi hilo ambalo lina lengo la kuondoa watumishi hewa ambao wamekuwa
wakijipatia fedha pasipo kufanya kazi.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment