Na John Gagarini, Kibaha
WANANCHI wa mtaa wa Mkombozi wilayani Kibaha mkoani Pwani
umeiomba Halmashauri ya Mji wa Kibaha kuwajengea kivuko au daraja kwenye mto
Mpiji kwa ajili ya kuvuka kwenda Majohe wilaya ya Kinondoni kupata huduma za kijamii
ambako ni jirani na ikilinganishwa na Maili Moja wilaya ya Kibaha umbali wa
kilometa zaidi ya 10.
Akizungumza na waandishi wa habari mkazi wa mtaa huo Malaki
Lakibuka alisema kuwa huduma hizo
wanazipata Majohe kutokana na ukaribu uliopo wa kilometa mbili ukilinganisha na
Kibaha ambako ni mbali kwa zaidi ya kilometa 10, lakini tatizo lililopo ni
kukosa kivuko au daraja.
Lakibuka alisema kuwa wako kwenye wakati mgumu kuvuka mto huo
kutokana na kuwa na mamba wengi jambo ambalo ni hatari kwa usalama wao ambapo
kwa miaka ya nyuma watu walikuwa wakiliwa na mamba.
“Tunapata taabu sana kuvuka hapo mtoni kwani mamba ni wengi
na pia endapo utapita vibaya unaweza kuchukuliwa na maji hasa wakati wa mvua
hivyo kuhatarisha maisha yetu na ikizingatiwa kuwa watumishi wanaofanya kazi
Majohe,” alisema Lakibuka.
Naye mweneykiti wa mtaa huo ambao ni mpya Moshi Mhagama
alisema kuwa kutokuwa na kivuko ni changamoto kubwa kwa wananchi ambao
wanategemea hali inakuwa mbaya kipindi cha
mvua ambapo mto huo unakuwa umejaa maji.
Moshi alisema kuwa wanategemea Majohe kama ni sehemu ya
kupata mahitaji yao ya kawaida ambako ni jirani ikilinganishwa na Kibaha ambako
ni mbali sana hivyo tungeomba Halmashauri iwasaidie ujenzi huo ambapo nao
tayari walishaanza kuchangishana fedha kwa ajili ya ujenzi wa kivuko.
“Kwa wagonjwa au mama wajawazito ni taabu kwani
wanajifungulia wakiwa njiani lakini pangekuwa na daraja wangepita kwa urahisi
na kuwawahisha wagonjwa kupata matibabu pia kuna wafanyakazi wanafanya kazi
ngambo ya pili ni shida sana kuvuka mvua zinapokuwa nyingi,” alisema Moshi.
Naye diwani wa kata hiyo Agustino Mdachi alisema kuwa jambo
hilo alilipeleka Halmashauri lakini alijibiwa kuwa uwezo wa kujenga daraja hilo
haupo kutokana na gharama za ujenzi kuwa kubwa sana kiasi cha zaidi ya bilioni
mbili.
Mdachi alisema kuwa changamoto kwenye eneo hilo ni kubwa sana
kwani mbali pia kuna mamba ambao ni hatari kwa watu wanaovuka hapo hivyo
kuhatarisha maisha yao.
“Mbali ya Halmashauri kusema kuwa hawana uwezo wa kujenga
daraja kwa sasa pia walisema hawawezi kujenga kivuko cha muda kwani gharama
itakuwa mara mbili wao wanataka wajenge kitu cha kudumu ambapo ni ujenzi wa
daraja,”alisema Mdachi.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment