Monday, May 23, 2016

VIONGOZI SIMBA WAWAJIBIKE


Na John Gagarini, Kibaha

UONGOZI wa Timu ya Soka ya Simba ya Jijini Dar es Salaam wametakiwa kuwajibika kutokana na matokeo mabaya ya timu kwenye mashindano ya Ligi Kuu ya Voda Com iliyomalizika mwishoni mwa wiki.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha msemaji wa Tawi la Simba Kibaha maarufu kama “Simba Tishio” Fahim Lardhi alisema kuwa viongozi hao wamekuwa wakiwawajibisha wachezaji pale wanapofanya vibaya hivyo na wao lazima wawajibike kwa hilo.

Lardhi alisema kuwa timu hiyo imefanya vibaya kwenye misimu minne na kuifanya timu hiyo ishindwe kushiriki michuano ya kimataifa kutokana na matokeo mabaya ambapo kwa msimu huu imeshika nafasi ya tatu.

“Timu ina vitengo vingi na kamati mbalimbali hivyo kama kuna kiongozi ambaye alizembea kwenye kitengo chake na kufanya timu ifanye vibaya kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake anapaswa kuwajibika kwa kuachia ngazi,” alisema Lardhi.

Alisema kuwa inasikitisha kuona timu inafanya vibaya kila mwaka ambapo kwa mwaka huu mwenendo wake haukuwa mzuri na kufanya timu kupata matokeo mabaya huku ikiwa imetambiwa na mtani wake Yanga kw akufungwa michezo yote.

“Tumechoka kusemwa vibaya na watani wetu hii ni fedheha kwetu tunaomba kiongozi yoyote ambaye alisababisha timu kufanya anapaswa kuwajibika kwa kuachia ngazi au kuondolewa,” alisema Lardhi.

Aidha alisema kuwa anawapongeza wanachama na wapenzi wa timu yao kwa kuwa na uvumilivu kwani kwa kipindi cha miaka minne timu yao imekuwa ikifanya vibaya lakini wametulia wakiamini kuwa timu itapata matokeo mazuri lakini imekuwa kinyume.

“Ligi imeshakwisha kila kiongozi atoe ripoti yake na kuonyesha uzaifu ulikuwa wapi ili kujipanga na msimu mwingine wa ligi ijayo ili timu ifanye vizuri na si kushika nafasi ambazo haiipi timu kushiriki michuano ya kimataifa,” alisema Lardhi.

Aliutaka uongozi kuwa makini katika usajili kwa kusajili wachezaji wenye uwezo na kuacha kusajili wachezaji wasio na uwezo kwani Simba inahitaji wachezaji wenye uwezo na si kila mchezaji anastahili kuichezea Simba kama ilivyokuwa kwa msimu huu kuwa na wachezaji wenye uwezo mdogo.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment