Na John Gagarini, Kibaha
WILAYA ya Mkuranga mkoani Pwani limechonga madawati 5,043 ili
kukabiliana na tatizo la upungufu wa madawati kwa wanafunzi wa shule za msingi
na sekondari.
Mkuu wa wilaya ya Mkuranga Abdala Kihato akisoma taarifa ya
wilaya hiyo kwa mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo wakati wa ziara
yake kutembelea wilaya hiyo kukagua shughuli za maendeleo.
Kihato alisema kuwa wilaya hiyo ilikuwa na upungufu wa
madawati 5,131 hivyo kubakiwa na upungufu wa madawati 500 ambayo wanatarajia
kukamilisha utengenezaji muda mfupi ujao.
“Tatizo la upungufu wa madawati kwa wanafunzi wa shule za
Sekondari tatizo hilo hakuna ila tatizo kubwa liko kwa wanafunzi wa shule za
Msingi kutokana na uwingi wao na hata wale wa darasa la kwanza ambapo kwa mwaka
huu walioandikishwa ni wengi sana,” alisema Kihato.
Alisema kuwa hawana wasiwasi kwani hadi ule muda uliowekwa wa
Juni 30 kwa wilaya zote kuondoa tatizo la wanafunzi kukaa chini litakuwa
limekwisha kabisa kwani wanashirikiana na wadau mbalimbali kutengeneza
madawati.
“Tunawahimiza watendaji wa vijiji na kata kuhakikisha
wanakamilisha zoezi hilo ili kuwaondolea adha wanafunzi kukaa chini na
kuwafanya washindwe kujifunza vizuri masomo yao,” alisema Kihato.
Aidha aliwaomba wadau wa maendeleo ndani ya wilaya hiyo
kuwaunga mkono katika kufanikisha zoezi hilo la uchongaji wa madawati kwa
wanafunzi kwenye wilaya hiyo.
Naye mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo alisema
kuwa anaipongeza wilaya hiyo kwa kuweza kufanikisha kuchonga madawati hayo
ambayo sasa yanaenda kuondoa tatizo hilo la upungiufu wa madawati.
Ndikilo alisema kuwa mkoa huo ulikuwa una upungufu wa
madawati 43,047 kwa shule za msingi lakini kwa jitihada hizo zitakuwa
zimepunguza kwa kiasi kikubwa upungufu huo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment