Thursday, May 19, 2016

MWENGE KUPITIA MIRADI YENYE THAMANI YA BILIONI 66.3

Na John Gagarini, Bagamoyo
MWENGE wa Uhuru jana ulianza mbio zake mkoani Pwani baada ya kumaliza kuzunguka mkoa wa Dar es Salaam ambapo utakimbizwa kwenye Wilaya Sita za mkoa huo na kupitia miradi 47 yenye thamani ya shilingi bilioni 66.3.

Akizungumza mara  baada ya kukabidhiwa mwenge  wa uhuru kutoka wilaya ya Temeke jijini Dar es salaam  mkuu wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo, alisema miradi hiyo imetekelezwa kwa ushirikiano wa serikali kuu na wananchi.

Ndikilo alisema kuwa kati ya miradi hiyo 47, miradi 14 itawekwa mawe ya msingi, 11 itazinduliwa,11 itafunguliwa na miradi mingine 11 itakaguliwa na mwenge huo utakapokuwa mkoani hapa.

 “Miradi mingine  imetekelezwa na Halmashauri, wahisani wa kitaifa na kimataifa pamoja na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ambapo ujumbe wa mwenge  mwaka huu unasema vijana ni nguvu kazi ya taifa na shirikisho la kuwezeshwa hivyo tupige vita matumizi ya madawa ya kulevya,” alisema Ndikilo.

Alisema kuwa kwa kutambua changamoto za vijana mkoa umejipanga katika kutatu  changamoto za vijana kwa ushirikiano na vijana wenyewe ambao katika mkoa huu wapo vijana 379,646 kati ya watu milioni 1.9.

“Mkoa umejipanga kutekeleza ujumbe huo kwa vitendo kwani  msingi mkubwa wa ujumbe ni vijana ndio nguzo na ni chachu kubwa ya maendeleo katika taifa hivyo lazima tuwape nafasi,” alisema Ndikilo.

Aidha aliwataka vijana kuchangamkia fursa za kiuchumi na kijamii zilizopo ili kujibu changamoto hususan za ajira walizonazo na ni wakati wa vijana kujitokeza kutumia fursa mbalimbali zikiwemo kujiajiri na kuwajibika ili kukabiliana na changamoto walizonazo kwa kuzigeuza kuwa fursa za ajira kwenye maeneo yao.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paulo Makonda akimkabidhi Ndikilo mwenge huo wa Uhuru alishukuru kukabidhi mwenge  huo kwa mkoa wa Pwani huku ukiwa umetembea mkoani kwake bila ya tatizo lolote na Mwenge leo  utakimbizwa katika wilaya ya Kibaha.

Mwisho


No comments:

Post a Comment