Na John Gagarini, Kibaha
KITUO cha Afya cha Mkoani kinakabiliwa na changamoto ya
ukosefu wa Jenereta ili kukabiliana na tatizo la ukatikaji umeme kwenye chumba
cha akinamama wanapojifungulia hivyo kuwaomba wadau mbalimbali.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na mganga mkuu wa Halmashauri ya
Mji wa Kibaha Happiness Ndosi wakati akipokea msaada wa vifaa mbalimbali kwa
watoto waliozaliwa na watakaozaliwa kutoka shirika lisilokuwa la kiserikali la
Abubaker Darwesh International Charitable Foundation (ADICF) la Jijini Dar es
Salaam.
Dk Ndosi alisema kuwa kukatika kwa umeme kwenye kituo hicho
ni changamoto kubwa hasa nyakati za usiku na wakati mama wajawazito wanapokuwa wanajifungua
hali ambayo inahatarisha maisha ya akinamama hao.
“Kutokana na hali hiyo tunawaomba wadau mbalimbali wajitokeze
kutusaidia kupata jenereta kwa ajili ya kusaidia mara umeme unapokatika katika
chumba cha uzalishaji mama wajawazito ili kunusuru maisha yao,” alisema Dk
Ndosi.
Aidha alisema mbali ya changamoto hiyo pia wanakabiliwa na
changamoto nyingine ikiwa ni pamoja na ukosefu wa chumba cha upasuaji, Ultra
Sound na X-Ray, gari la wagonjwa kwani lililopo ni chakavu, magodoro na vitanda
hasa ikizingatiwa kuwa kituo hicho kiko mbioni kuwa Hospitali ya Wilaya.
Kwa upande wake mwanzilishi na meneja mradi wa shirika hilo
Bilal Abubekar alisema kuwa shirika lake limeamua kutoa misaada hiyo kwa lengo
la kuisaidia jamii hasa kwa watoto wadogo wenye umri chini ya miaka mitano ili
kuisaidia serikali kuhakikisha watoto chini ya miaka mitano wanapata huduma
bora.
Abubaker alisema kuwa shirika lao limekuwa likisaidia makundi
mbalimbali ikiwa ni pamoja na wajane yatima na watu wenye mahitaji, pia
kusaidia elimu watu wenye ulemavu.
Naye moja ya wagonjwa waliopata msaada huo Mariamu Ally alishukuru
shirika hilo na kusema kuwa wameonyesha moyo wa upendo na kuwataka waendelee
kusaidia hospitali hiyo ili iweze kukabiliana na changamoto zilizopo kwa
wagonjwa.
Alisema kuwa moja ya changamoto iliyopo kwenye wodi hiyo ni
kuchanganywa kati ya akinamama waliojifungua na wale wanaosubiri kujifungua na
kutaka watu hao kutenganishwa ili kila moja wawe na sehemu yao.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment