Na John
Gagarini, Kisarawe
SERIKALI imeombwa kusaidia vikundi
vya vijana vinavyopata mafunzo mbalimbali ya kuwainua kiuchumi ili waweze
kujiajiri wakiwa Vijijini badala ya kukimbilia Mijini.
Akisoma risala ya wahitimu mbele ya
mgeni rasmi ambaye ni kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa George Mbijima kwenye
Kijiji cha Kibuta wilayani Kisarawe, Mariam Christopher alisema kuwa mafunzo
hayo yatawawezesha kuweza kukabili mazingira wanayoishi huko huko waliko kuliko
kukimbilia mjini kutafuta ajira.
Christopher alisema kuwa masomo
waliyojifunza ni ya ufundi kwa vijana wa kata ya Kurui kupitia mradi wa
kuwajengea uwezo vijana (YEE) unaosimamiwa na shirika lisilokuwa la kiserikali
Plan International wilaya ya Kisarawe.
“Tunashukuru wafadhili wetu kwani
tumeweza kujifunza mambo mengi ya ufundi tunaamini yatatusaidia tukiwa huku
huku bali kikubwa ni Halmashauri kutuwekea mazingira mazuri ya kufanya kazi ili
tuisaidie jamii ya Kijijini hasa ikizingatiwa nako kuna hitaji maendeleo,”
alisema Christopher.
Alisema kuwa mafunzo hayo wameyapata
kwa kina katika fani mbalimbali za upambaji, mapishi, udereva, ushonaji na
utengenezaji wa mapambo na wanatarajia kuboresha shughuli hizo Vijijini ili
kuleta maendeleo kwa familia zao na wao binafsi.
Aidha alisema kuwa mafunzo hayo
yanafadhiliwa na Eu, Vso, Uhiki, Veta na Plan International wilayani humo na
yanatekelezwa kwenye kata Sita za Kibuta, Kisarawe, Manerumango, Msimbu, Kurui
na Marumbo na yanatarajiwa kuwafikia vijana 1,000 kwa kipindi cha miaka mitatu.
Kwa upande wa kiongozi wa mbio za
mwenge Kitaifa George Mbijima alisema kuwa Halmashauri inapaswa kuwatengenea
vijana asilimia tano ya mapato yao kwa ajili ya kuwakopesha vijana kwani suala
hilo liko kisheria na wanapaswa kutekeleza ili kuwajenga vijana kiuchumi, Mwenge
huo leo unatarajiwa kukimbizwa wilaya ya Rufiji.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment