Na John Gagarini, Kibaha
IMEELEZWA kuwa dhana ya Mwenge wa Uhuru si itikadi ya chama
au watu wa aina fulani bali ni kuhamasisha maendeleo ya wananchi kupitia miradi
ambayo imetokana na nguvu zao.
Hayo yalisemwa wilayani Kibaha na kiongozi wa mbio za Mwenge
Kitaifa George Mbijima alipokuwa akizindua bweni la wasichana kwenye Shule ya
Sekondari ya Zogowale wakati mwenge huo ukikimbizwa wilayani humo.
Mbijima alisema kuwa Mwenge wa Uhuru ni alama ya maendeleo
katika nchi ambapo mwasisi wake Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliutumia kama
ishara ya maendeleo.
“Mwenge ni alama muhimu katika maendeleo ya nchi kwani kila
mahali ulipopita umeacha alama ya maendeleo na lengo lake ni kuhamasisha watu
kuwa wanapaswa kuwajibika ili kuleta mafanikio kwa mtu mmoja mmoja na jamii
nzima kwa jumla,” alisema Mbijima.
Alisema kuwa watu wanaobeza Mwenge hawajui historia ya nchi
na umuhimu wa mwenge ambacho umezindua na kufungua miradi mingi ya maendeleo
ambayo imewaletea watu mafanikio.
“Sehemu yoyote ambayo mwenge umepita umeleta mafanikio
kutokana na miradi iliyopo na kufunguliwa au kuzinduliwa na mbio hizi ambazo
hufanyika kila mwaka,” alisema Mbijima.
Aliwaasa wanafunzi kuzingatia masomo na kuacha kujiingiza
kwenye mambo ambayo yatawaharibia masomo yao ikiwa ni pamoja na matumizi ya
dawa za kulevya au kushiriki kwenye vitendo vya ngono ambavyo mwisho wake ni
kupata maambukizi ya magonjwa mbalimbali ukiwemo ukimwi.
Awali akisoma risala kwa mgeni rasmi mwalimu mkuu wa shule
hiyo tatu Mwambala alisema kuwa ujenzi huo ulianza mwaka 2015 na kukamilika
mwaka mwaka huo huo na kugharimu kiasi cha shilingi milioni 230,814,608.
Mwambala alisema kuwa lengo la ujenzi huo ni kuweka mazingira
rafiki ya kujifunza na kujifunzia kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita ili
kuongeza ufaulu ambapo bweni hilo lina uwezo wa kulaza wanafunzi 86 na lina
miundombinu yote. Shule hiyo ilianzishwa mwaka 2007 na ilipata kibali cha
kuanzisha kidato cha tano na sita mwaka 2014 na ina wanafunzi 408.
Mwenge huo ukiwa wilayani Kibaha ulitembelea miradi
mbalimbali yenye tahamani ya shilingi zaidi ya bilioni nne leo unakimbizwa
wilayani Mkuranga kuendelea na mbio zake.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment