Na John Gagarini, Kisarawe
SERIKALI itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wa
ndani na nje ambao watafuata taratibu za nchi ili kuongeza pato la taifa
kupitia sekta ya uwekezaji ambayo kwa sasa inakuwa kwa kasi kwenye mikoa
mbalimbali.
Hayo yalisemwa na kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa George
Mbijima alipokuwa akiweka jiwe la msingi kwenye Bandari ya Nchi Kavu
inayojengwa kwenye Kijiji cha Kazimzumbwi wilayani Kisarawe mkoani Pwani.
Mbijima alisema kuwa nchi kwa sasa iko kwenye kipindi cha
utekelezaji kwa vitendo sera ya
uwekezaji ili iweze kuleta manufaa kwa wananchi pamoja na serikali ili iweze
kuwaletea maendeleo wananchi kupitia uwekezaji.
“Serikali inathamini mchango wa wawekezaji kwani wana nafasi
kubwa ya kuleta maendeleo kwa wananchi pamoja na nchi lakini kikubwa ni kuwa
wazi wakati wa kufanya taratibu za uwekezaji ili kuondoa malumbano
yanayojitokeza baina ya wananchi na wawekezaji,” alisema Mbijima.
Alisema kuwa baadhi ya wawekezaji wamekuwa wakikiuka taratibu
za uwekezaji kwa kutokuwa wazi wakati wakufanya michakato ya uwekezaji kwani
wanapaswa kuwa wazi kwa pande zinazohusika ili kuondoa mikanganyiko.
“”Wawekezaji wanapaswa kufuata sheria za nchi zilizowekwa ili
faida inayopatikana iweze kuleta manufaa kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya
uwekezaji hivyo wanapaswa kushirikiana na wananchi ili kuondoa migogoro isiyo
na tija kwa uwekezaji”, alisema Mbijima.
Aidha alisema kuwa serikali inatoa ushirikiano na wawekezaji
kwnai mbali ya kutoa ajira kwa wananchi pia serikali inapata mapato yake
kupitia sekta hiyo ili iweze kuendesha shughuli zake kupitia kodi na ushuru
mbalimbali.
Kwa upande wake mkurugenzi wa Kampuni ya DSM Corridor Group Sada Shaban alisema kuwa ujenzi huo wa Bandari
kavu ulianza 2013 na kukamilika mwaka huu kwa baadhi ya vitengo ukiwa
umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 7.5 ambapo gharama iliyobakia ni kiasi
cha shilingi bilioni 38 hadi kukamilika kwake.
Shaban alisema kuwa eneo hilo litakuwa ni hifadhi ya bidhaa
mbalimbali ikiwa ni pamoja na maghala ya mazao mbalimbali, madini na mizigo ya
kila aina na itasaidia kupunguza msongamano barabarani kwani ikitoka hapo
inapakizwa kwenye treni ambayo iko jirani na bandari hiyo. Mwenge huo ukiwa
wilayani Kisarawe ulizindua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi yenye
thamani ya shilingi bilioni 6.5 leo mwenge unakimbizwa wilayani Rufiji.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment