Na John Gagarini, Kibaha
JESHI la Polisi Mkoani Pwani bado
linaendelea kumtafuta mwanafunzi wa shule ya Sekondari ya Rafsanjani iliyopo
Soga Tarafa ya Mlandizi wilayani Kibaha mkoani Pwani baada ya kuchoma bweni la
wasichana la shule hiyo.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani
Pwani Bonaventura Mushongi alisema kuwa mwanafunzi huyo ambaye hakuweza
kufahamika alichoma bweni hilo juzi majira ya saa 4 usiku liitwalo Umoja.
Mushongi alisema kuwa hata hivyo tukio
hilo halikuwa na madhara kwa wanafunzi zaidi ya kuharibu mali zilizokuwa kwenye
bweni hilo ambazo hata hivyo thamani yake haikuweza kufahamika mara moja.
“Tunaendelea kumfuatilia mwanafunzi
huyo ili tuweze kumjua na kumchukulia hatua za kisheria lakini hadi sasa bado
hatujafanikiwa kumpata kwani aliandika kwenye sanduku la maoni juu ya dhamaira
yake hiyo mbaya ya kuchoma bweni,” alisema Mushongi.
Alisema kuwa wanaendelea kuzifanyia
kazi taarifa hizo ili waweze kumbaini mwanafunzi huyo ili hatua kali za
kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yake kwani kitendo alichokifanya ni cha
hatari kwa maisha ya wanafunzi wenzake na mali.
“Tunatoa wito kwa wanafunzi wanapokuwa
shuleni wazingatie masomo na kuachana na vitendo visivyo kuwa na maadili kwani
jeshi halitawavumilia wanafunzi ambao wanabainika kufanya vitendo viovu kwani
tutawakamata na kuwapeleka kwenye vyombo vya sheria ikiwa ni pamoja na
mahakamani,” alisema Mushongi.
Bweni hilo lilichomwa moto juzi na
mwanafunzi huyo lakini hata hivyo kikosi cha zimamoto mkoa wa Pwani polisi
pamoja na wananchi walifanikiwa kuzima moto huo na haukuweza kuleta madhara kwa
wanafunzi.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment