Na John Gagarini, Msoga
MKOA wa Pwani umeunda tume kufuatilia maradi wa Skimu ya Umwagiliaji wa Bwawa hilo lililopo Kijiji cha Msoga kata ya Msoga wilaya ya Bagamoyo ambalo ujenzi wake umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 2 kwa kipindi cha zaidi ya miaka 10 bila ya kukamilika.
Akizungumza jana baada ya kufanya ziara kwenye mradi huo wa umwagiliaji mkuu wa Mkoa wa Pwani, Injinia Evarist Ndikilo alisema kuwa fedha zilizotumika ni nyingi lakini hakuna kinachoendelea na bado zinahitajika fedha nyingine ili kuukamilisha mradi huo.
Mradi huo ambao unasimamiwa na Halmashauri na Wizara ya Maji na Umwagiliaji Tume ya Umwagiliaji Kanda ya Mashariki ambayo makao yake makuu mkoani Morogoro umeshindwa kukamilika katika kipindi hicho huku kiwango kikubwa cha fedha kikiwa kimetumika.
Ndikilo alisema kuwa thamani ya fedha na mradi haviendani hivyo kuna haja ya kuufuatilia kwa kina mradi huo ambao ni mali ya wananchi wa kijiji hicho ambao ulilenga kuendesha kilimo cha umwagiliaji, maji kwa ajili ya kunywa kunyweshea mifugo, ufugaji wa samaki na kilimo cha mbogamboga.
Akielezea kuhusu mradi huo mhandisi mkazi wa kanda wa ofisi ya umwagiliaji Idd Said alisema kuwa mradi huo ulianza mwaka 2009 kwa uchimbaji wa Bwawa ambalo lilikamilika mwaka 2010 kwa gharama ya shilingi bilioni 1,697,444,266 kwa ajili ya tuta kubwa la bwawa, sehemu ya utoro, bomba kuu pamoja na chemba zake na birika la kunyweshea mifugo.
Said alisema kuwa mkataba wa pili ulisainiwa mwaka 2011 hadi mwaka 2012 na ulikuwa na thamani ya shilingi milioni 350,000,000 kwa ajili ya miundombinu ya umwagiliaji ambapo mkataba huu ulivunjwa kwa makosa ya mkandarasi kabla ya kazi kukamilika ambapo Halmashauri iliingia mkataba na mkandarasi mwingine ambaye hata hivyo naye alishindwa kukamilisha kazi hiyo.
“Kutokana na ujazo wa bwawa kuwa mdogo halmashauri iliomba kupata fedha nyingine tena kiasi cha shilingi milioni 300,000,000 kwa ajili ya kuchimba visima virefu ili kupata maji zaidi ya umwagiliaji kwa njia ya matone hata hivyo maji hayakupatikana katika visima vitatu vilivyochimbwa kwa urefu wa hadi mita 180,” alisema Said.
Alisema kuwa Halmashauri iliomba kubadilishiwa matumizi ya fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya mikataba hiyo ya awali na kuhamishiwa katika kazi ya sasa ya ujenzi wa kuongeza ukubwa wa bwawa kutoka mita za ujazo 427,600 hadi mita za ujazo 970,480 kwa ajili ya matumizi ya hekari 125.
“Baada ya changamoto hizo mkandarasi wa sasa ambaye ni wa tatu anaendelea na kazi aliingia mkataba wa shilingi milioni 915, 648 494 ambapo fedha aliyolipwa hadi sasa ni shilingi milioni 135,340,444 na mkataba huu ulisaini mwaka 2015 na alitakiwa kumaliza Machi 2016 lakini hadi sasa hajamaliza kazi na kuomba kuongezewa muda hadi Aprili 30 lakini hakukamilisha kazi,” alisema Said.
Alisema kuwa changamoto kubwa ya kazi hiyo ni kutokana na udongo unaotumika kuwa wa mfanyinzi ambao ukipata mvua kidogo unanata na kuwa vigumu kuchimba na kuubeba udongo huo.
Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo Marry Kisimbo alisema kuwa mradi huo umekumbwa na changamoto ya awakandarasi kushindwa kukamilisha kazi kwa madai ya udongo kuwa mbaya pale inaponyesha mvua.
Naye ofisa kilimo wa wa Halmashauri hiyo dionis mahilane alikiri kuwepo na tatizo katika utekelezaji wa mradai huo na kusema kuwa kwa upande wa malipo wakandarasi walilipwa kutokana na kazi waliyoifanya.
Kutoakana na maelezo hayo mkuu wa mkoa alisema kuwa haridhiki na maelezo hayo kwani haiwezekani kama bwawa lilishakamilika kwanini hawakuanza kutumia maji yaliyopo lakini wao wakataka kuongeza chanzo kingine cha maji.
Ndikilo alisema kuwa mradi huo unaonekana kuna dalili za matumizi mabaya ya fedha kwani haiwezekani mradi huo ushindwe kukamilika kwa kipindi cha miaka 10 wakati serikali na wadau wa maendeleo walikuwa wakitoa fedha kwa ajili ya mradi huo.
“Wote waliohusika na mradi huu hata kama wamehamishwa au wako masomoni wanapaswa kuja kutoa maelezo juu ya fedha hizi zilizotumika hapa hata wale wa halmashauri ambao wlaikuwa wakiwalipa wakandarasi ambao wamekuwa hawamalizi kazi na kuondoka baada ya kulipwa kwa watakaobainika kuwa walihujumu mradi huu sheria kali zitachukuliwa dhidi yao baada ya tume itakayoanza kazi kuanzia sasa na baada ya wiki watanipa majibu baada ya uchunguzi kuangalia kama kuna ubadhirifu,” alisema Ndikilo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment