Na John Gagarini, Kibaha
SAKATA la Mwenyekiti wa Mtaa wa Muheza wilayani Kibaha mkoani
Pwani Maulid Kipilili limechukua sura mpya baada ya wananchi wa mtaa huo
kumkataa mwenyekiti huyo kwenye mkutano wa wananchi uliofanyika mtaani hapo.
Wananchi hao walimkataa mwenyekiti wao wakati wa mkutano
ulioitishwa na diwani wa kata ya Maili Moja Ramadhan Lutambi ili kujadilia
suala la malalamiko ya wananchi wa mtaa huo baada ya kuifunga ofisi ya mtaa
hadi pale watakapofikia muafaka juu ya mwenyekiti wao.
Mkutano huo ambao ulifanyika mtaani hapo chini ya diwani huyo
wa kata na ofisa Mtendaji wa Kata hiyo Thadeo Mtae wananchi hao walilalamika
kuwa mwenyekiti wao tangu achaguliwe kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika mwishoni
mwa mwaka 2015 hajaitisha mkutano wa wananchi.
Kabla ya kufikia hatua ya kumkataa mwenyekiti wao wananchi
hao walitoa malalamiko yao mbalimbali ikiwa ni pamoja na kulalamika kuwa
mwenyekiti wao haitishi vikao vya wananchi, hasomi mapato na matumizi,
kutofungua ofisi hivyo kuwapa shida wananchi wanapokwenda kupata huduma za
kiofisi.
Akizungumza juu ya mwenyekiti wao kushindwa kuwajibika mwananchi
wa mtaa huo Kitai Mganga alisema kuwa ni pamoja na tuhuma nyingine ni kushindwa
kusimamia mali za mtaa ikiwa ni pamoja na baadhi ya watu kumega na kuuziana
eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa shule ya Msingi lakini hakuna hatua
zozote ambazo amezichukuwa.
“Mtaa wetu una changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na ukosefu
wa maji, umeme, Shule ya Msingi, bararabara na zahanati lakini kutokana na
mwenyekiti wetu kutowajibika tumeshindwa kufanya lolote hata kuweka mikakati ya
maenedeleo hakuna,” alisema Mganga.
Naye Paulo Chacha alisema kuwa mwenyekiti lazima awe na
wajumbe wa mtaa lakini cha kushangaza wajumbe hawapo hivyo mwenyekiti anafanya
kazi peke yake jambo ambalo haliwezi kuleta mafanikio.
Chacha alisema kuwa kamati ya mtaa ni sawa na baraza la mawaziri
sasa haiwezekani Rais kuongoza nchi bila ya kuwa na Mawaziri kwani maendeleo
hayawezi kupatikana.
Kwa upande wake Maulid Kipilili alisema kuwa kwa upande wa
mikutano alishindwa kufanya kutokana na sababu maalumu ikiwa ni pamoja na
shughuli za kitaifa.
Kipilili alisema kuwa aliitisha mikutano mitatu ya dharura na
miwili ya kikatiba na kuwashangaa wananchi hao kumsingizia kuwa hajafanya
kabisa mikutano na mmoja wa Mei 15 ulishindwa kufanyika kutokana na akidi
kushindwa kuenea.
“Kuhusu wajumbe wa serikali ya mtaa hawajafika kwa sababu
mbalimbali lakini wapo na sina mgogoro na wajumbe wangu na tunafanya kazi
vizuri na baadhi ya kamati zipo na zinafanya kazi kama ya maji na shule zipo na
aliyeuziwa eneo la shule kama kuna mtu anaushahidi alete ili tuchukue hatua za
kisheria,” alisema Kipilili.
Akielezea juu ya changamoto hiyo ya wananchi kumkataa
mwenyekiti wao diwani wa kata hiyo Ramadhan Lutambi alisema kuwa kama hawamtaki
wanapaswa kufuata taratibu kwani hatua ya kwanza ni hiyo.
Lutambi alisema kuwa kutokana na hali hiyo itabidi uitishwe
mkutano wa dharura wa kata kujadili suala hilo na wao ndiyo watakaoamua hatma
ya mweneyekiti wao.
Kufuatia kukataliwa na wananchi ofisa mtendaji wa kata ya
Maili Moja Thadeo Mtae alisema kuwa hoja zilizotolewa ni 15 ambapo zimejibiwa
na mwenyekiti huyo ambapo baadhi wamekataa majibu yake na nyingine wamekubali
majibu.
Mtae alisema kuwa atapeleka sehemu husika kwa ajili ya majibu
na hatua zaidi kwani yeye hatoweza kutoa majibu hivyo wasubiri majibu ambapo
kutaitishwa mkutano mwingine.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment