Thursday, May 5, 2016

MADIWANI WATAKA BODI YA TENDA IVUNJWE

Na John Gagarini, Kibaha
MADIWANI wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani wameridhia kuvunjwa kwa Bodi ya Tenda kwa kushindwa kutekeleza vizuri majukumu yake hivyo kusababisha miradi mingi kukwama.
Wakizungumza kwenye kikao cha Madiwani kilichofanyika mjini Kibaha madiwani hao walisema kuwa kutokana na bodi hiyo kutokuwa makini imesababisha wakandarasi wengi kuidai Halmashauri huku miradi mingi ikiwa imejengwa chini ya kiwango.
Akizungumza kwenye kikao hicho Diwani wa Kata ya Tumbi Hemed Chanyika alisema kuwa wazabuni wengi wameingia kwenye mgogoro na Halmashauri kwani wengi wameshindwa kufikia vigezo vya kazi wanazopewa huku mawakala wakishindwa kupeleka fedha za makusanyo kwa wakati.
Chanyika alisema kuwa bodi hiyo imeshindwa kuchagua wazabuni ambao wana uwezo wa kufanya kazi na inafanya kazi kwa mazoea pia ni ya muda mrefu hivyo inapaswa kubadilishwa ili kuleta ufanisi katika utendaji kazi kwa wazabuni kwa lengo la kuleta maendeleo.
“Baadhi ya miradi mingi imekwama kwani wazabuni wengine wameshindwa kukamilisha kazi zao wengine wamekuwa wakiachia kazi bila ya kukamilika na kuondoka matokeo yake ni kuitia hasara Halmashauri na kudumaza maendeleo ya Mji wetu,” alisema Chanyika.
Kwa upande wake Kambi Legeza alisema kuwa miradi mingi iko chini ya kiwango kutokana na kutokuwa na wakandarasi wasiokuwa na uwezo pia mapato ya Halmashauri yameshuka hivyo kuna haja ya kuibadili ili kupata bodi nyingine itakayokuja na mawazo mapya.
Legeza alisema kuwa bodi hiyo ya tenda ndiyo yenye uwezo wa kuwapitisha wazabuni mbalimbali ambao wanapaswa kuwa na uwezo lengo likiwa ni kuleta maendeleo kwa halmashauri ambayo yanaleta manufaa kwa wananchi ambao ndiyo wanaolengwa.
Akijibu hoja hizo kaimu mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Leah Lwanji alisema kuwa ofisi yake imelipokea suala hilo na italifanyia kazi kama mapendekezo ya madiwani yalivyotolewa.
Lwanji alisema kuwa kuna taratibu za kisheria za kuvunja bodi hivyo lazima zifuatwe na endapo itabidi kufanya hivyo itafanyika ili kuhakikisha taratibu zinafuatwa kwa lengo la kuboresha.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment