Thursday, May 5, 2016

WATAKA VYUO VYA KATI KUUNGANISHWA NA BODI YA MIKOPO

Na John Gagarini, Kibaha

SERIKALI na Bodi ya Mikopo Nchini (TCU) imeshauriwa kuviingiza kwenye mpango wa mikopo wanafunzi wanaosoma Vyuo vya Kati kama ilivyo kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu.

Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani Abdul Sharifu wakati mkutano wa Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo vya Juu wa (CCM).

Sharifu alisema kuwa wanafunzi hao ni sawa na wale wa vyuo vikuu na wengine wanatoka kwenye mazingira magumu na wanahitaji mikopo ili waweze kupata elimu ya juu.

“Hali ya sasa ni ngumu na wazazi ni wale wale wanahitaji kupunguziwa mzigo wa kulipa ada ambazo ni kubwa hivyo tunaona kuwa kuna haja ya serikali kuviingiza na vyuo vya kati kwenye mpango wa kutoa mikopo kwa wanafunzi,” alisema Sharifu.

Alisema kuwa kwa kuwa nchi imeamua kuwekeza kwenye elimu kwa lengo la kuhakikisha kuwa watoto wanapata elimu bora hadi kufikia elimu ya juu ambayo ndiyo inaweza kumsaidia mtoto.

“Kwa sasa elimu ya juu ndiyo inayotakiwa tofauti na elimu ya kawaida ambayo si ya juu ambayo kwa sasa haina nafasi ya muhitimu kupata ajira hivyo kulazimisha watu wapate elimu ya juu,” alisema Sharifu.

Aidha alisema kuwa shirikisho hilo ni mboni ya chama na linafanya kazi kubwa ya kukijenga chama kwani hapo ni tanuru la kuandaa viongozi wa baadaye wa kukiongoza chama pamoja na nchi.

Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kibaha Maulid Bundala  ambaye alimwakilisha mwenyekiti wa Mkoa Mwinshehe Mlao alikuwa mgeni rasmi kwenye mkutano huo alisema kuwa Shirikisho la Vyuo Vikuu la CCM linafanya kazi kubwa ya kukitetea chama.

Bundala alisema kuwa CCM imeleta ukombozi ndani ya nchi na ni chama kikongwe hivyo kwa wanavyuo waliojiunga na shirikisho hilo wako sehemu salama kwani mawazo yao yataleta manufaa kwa nchi.

Aidha alisema kuwa nchi kwa sasa ina hitaji kuongozwa na wasomi hivyo wasomi hawa wataleta mabadiliko na chama kiko tayari kubadilika na wao wananafasi ya kumshauri Rais na wao ndiyo watakaoliinua taifa.

Naye naibu katibu mkuu wa shirikisho hilo Siraji Madebe alisema kuwa shirikisho lao linakabilia na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na wancahama wake wale wa vyuo vya kati kutotambuliwa na Bodi ya Mikopo hivyo kutopata mikopo.

Madebe alisema kuwa licha ya changamoto mbalimbali lakini watahakikisha wanaendeleza umoja wao ili kufanikisha malengo ya kuanzishwa shirikisho hilo ambayo ni kuwaunganisha wasomi walio vyuo kuwa na umoja wao ili kukipigania chama.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment