Na John Gagarini, Kibaha
BAADHI ya wakazi kwneye eneo la Sagulasagula maarufu kama
Loliondo Mtaa wa Machinjioni kata ya Tangini wilayani Kibaha mkoani Pwani
wanaodaiwa kuvamia eneo lililotengwa kwa ajili ya soko wameiomba Halmashauri ya
Mji kuwalipa fidia na maeneo ya kuishi baada ya kupewa siku 14 kuhama kwenye
eneo hilo.
Wakizungumza mara baada ya kamati ya ulinzi na usalama ya
Wilaya kupitia na kuangalia eneo hilo na kutoa maagizo kwa wakazi hao kubomoa
nyumba zipatazo 55 zilizojengwa kwenye eneo hilo walisema kuwa kwa kuwa ni
mpango wa maendeleo basi nao waangaliwe kwani wamekaa hapo kwa muda mrefu.
Said Tekelo alisema kuwa baadhi ya watu wako hapo tangu mwaka
1970 na mwaka 2003 Rais Benjamin Mkapa wakati ule alifuta hati ya eneo hilo
toka eneo la Viwanda na kutaka lirejeshwe kwenye mtaa kwa ajili ya matumizi
mengine.
“Baada ya kurejeshwa kwenye mtaa baadhi ya watu walipimiwa
maeneo yao baada ya kupigwa picha na kamahaitoshi hata alipokuja waziri wa
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alitoa miezi mitatu sasa sita Halmashauri
ikae na wakazi hao ili kujadili namna nzuri ya kufanya,” alisema Tekelo.
Alisema kuwa licha ya maagizo hayo walikwenda Mahakamani
kwenda kulalamika walipotakiwa kuondoka na kesi iliendeshwa na wao kushindwa na
Mahakama ili amuru Halmashauri ikae nao lakini hakuna kilichofanyika hadi
mwishoni mwa wiki walipotakiwa kuvunja wenyewe na endapo hawatafanya hivyo
Halmashauri itabomoa nyumba hizo.
“Tumeambiwa tubomoe wenywe na kuanzia leo Tanesco na Dawasco
wameshapewa maagizo ya kuondoa miundombinu yao ilkiwa ni maandalizi ya kubomoa
sisi tunaomba Halmashauri itufikirie kwa kutulipa fidia pamoja na maeneo kwa
ajili ya kuishi kwani wenzetu jirani ambao tuko kwenye mgogoro mmoja wamelipwa
na kupewa viwanja,” alisema Tekelo.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Tangini Theodori Joseph
alisema kuwa suala hilo ni la muda mrefu ambapo baraza la Madiwani miaka ya
nyuma waliwatambua wakazi hao kutaka walipwe fidia na walikuwa wakishirikiana
nao katika mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuchukua kodi za majengo.
Joseph alisema kuwa kuna haja ya Halmashauri kuwafikiria
wakazi hao kwani wengine wako hapo miaka 40 iliyopita na wameendeleza ardhi kwa
kipindi chote hicho lakini jirani zao ambao wametengwa na barabara wao wamepewa fidia na watapewa viwanja.
Ofisa Habari wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Inocent
Byarugaba alisema kuwa eneo hilo lilitengwa kwa ajili ya soko na liko kwenye
Ramani ya Mji na wakazi hao walilivamia
eneo hilo na wanapaswa kuliachia.
Byarugaba alisema kuwa tayari eneo hilo liko kwenye
maandalizi ya ujenzi wa soko unatarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa
kwani tayari ramani imeshatoka ambapo soko linalotumika kwa sasa liko kwenye
hifadhi ya barabara na litabomolewa muda wowote na Tanroads.
Naye kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri Lucy Kimoi alisema kuwa
wakazi hao wanapaswa kuondoka na kwa sasa wanaandaa notisi kwa ajili ya
kuwataka waliachie eneo hilo kwani wako hapo kinyume cha Sheria.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment