Na John Gagarini, Kibaha
WANANCHI wa Mitaa ya Viziwaziwa na Sagale wilayani Kibaha
mkoani Pwani wataondokana na adha ya ukosefu wa Maji baada ya mradi mkubwa wa
maji wenye thamani ya shilingi 517,110,110 kuzinduliwa na kiongozi wa mbio za
Mwenge Kitaifa George Mbijima.
Mradi huo utakaohudumia wakazi 1,482 umekamilika baada ya
Halmashauri kuomba maji kwenye bomba kuu la Mamlaka ya Maji Safi na Maji taka
Dar es Salaam (DAWASCO) la Ruvu Juu baada ya majaribio ya kuchimba visima vya
ardhini ambavyo havikupata maji.
Akielezea juu ya mradi huo katibu wa Jumuiya ya Watumiaji
Maji wa Ziwaziwa na Sagale (SAVI) Abdulrahman Mango alisema kuwa mradi huo ni
moja ya miradi ya Maji na Usafi wa Mazingira ni moja wapo ya mitaa minne
iliyopo kwenye kata ya Viziwaziwa ambako katika Halmashauri kwenye miradi hiyo
kuna jumla ya mitaa 13.
“Kabla ya kuwa na mradi huu tulikuwa tunategemea maji ya
visima vya asili ambavyo ni vya msimu ambapo maji tuliyokuwa tukiyatumia
yalikuwa siyo safi wala salama na inapofikia wakati wa kiangazi tunakwenda
kuchota maji kwenye mtaa jirani wa Kwa Mfipa uliopo kilomita saba na
kuwachukulia wananchi muda mwingi kutafuta maji badala ya kufanya shughuli za
maendeleo,” alisema Mango.
Mango alisema kuwa mradi huo una husisha ujenzi wa tanki la
chini lenye ujazo wa lita 50,000, ujenzi wa chumba kwa ajili ya kuweka pampu,
uchimbaji wa mitaro na ulazaji wa mabomba, tanki la juu lenye ujazo wa lita
50,000, ujenzi wa vituo 10 vya kuchotea maji na ujenzi wa mifumo matanki ya
uvunaji wa maji ya mvua.
“Ujenzi wa miundombinu ya umekamilika na kwa sasa vituo tisa
kati ya 10 vinatoa huduma ya maji kwa mgao wa DAWASCO siku mbili kwa wiki na
unasimamiwa na SAVI na jamii huchangia shilingi 100 kwa ndoo ya lita 20 ambapo
fedha hupelekwa benki na hadi sasa kuna akiba ya shilingi 950,000 na fedha
zinazopatikana hutumika kwa ajili ya kulipia bila ya umeme, kufanya ukarabati
mdogomdogo, uendeshaji wa ofisi na kulipa bili ya DAWASCO,” alisema Mango.
Aidha alisema kuwa mradi huo umechangiwa na wananchi kiasi
cha shilingi milioni 12 kwa kutoa maeneo yao na kupitisha mabomba na kujenga
vituo vya maji vya jamii na kutekeleza azma ya Rais Dk John Magufuli ya kumtua
mama ndoo kichwani.
Kwa upande wake kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa Mbijima
alisema kuwa azma ya serikali ni kuwapunguzia kero wananchi kwa kupata huduma
za kijamii karibu ili wapate muda mwingi wa kufanya shughuli za maendeleo na si
kutumia muda mwingi kutafuta huduma.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment