Thursday, May 12, 2016

KIWANDA CHA TILES KUJENGWA MKURANGA


Na John Gagarini, Mkuranga
WAKAZI wa mkoa wa Pwani wametakiwa kuunga mkono mkakati wa serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Dk John Magufuli ya kuhamasisha ujenzi wa viwanda na uwekezaji.
Akizungumza na wakazi wa vijiji vya Nyamato na Mkiu wilayani Mkuranga wakati alipotembelea kiwanda cha kutengeneza vigae (Tiles) cha Goodwill Tanzania Ceramic mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo alisema kuwa wananchi wananafasi kubwa ya kufanikisha nchi kuwa ya viwanda kwa kushirikiana na wamiliki wa viwanda.
Ndikilo alisema kuwa wananchi wanapaswa kuwapa ushirikiano wawekezaji wa viwanda ili waweze kufanya kazi bila ya kuhujumiwa kwani kuna baadhi ya watu wamekuwa wakihujumu miundombinu ya viwanda.
“Wawekezaji kama hawa wa viwanda mnapaswa kuwaunga mkono kwani manufaa ya uwepo wao ni mengi sana ikiwa ni pamoja na kupata ajira pamoja na nyie kuuza bidhaa zenu kwani biashara zitakuwa nyingi hivyo mtaweza kubadilisha maisha yenu lakini endapo mtawafanyia vitendo vya kuwakatisha tama wataondoka,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa kwa sasa mkoa wa Pwani ajenda yake ni kuhakikisha unakuwa mkoa wa viwanda na hilo linawezekana kwa kuwa na viwanda vingi vya kuzalisha bidhaa mbalimbali.
“Mkoa kwa sasa umeamua kujitangaza kiviwanda kwnai nafasi za uwekezaji bado zipo nyingi na lengo ni kuhakikisha wananchi wanakuwa na uchumi wa kati na utainuka endapo kutakuwa na viwanda vingi mfano tu wilaya ya Mkuranga mmeanza kutekeleza kwa vitendo mkakati wa Rais wa kuwa na viwanda kwnai kwa sasa kuna viwanda 59,” alisema Ndikilo.
Aliwataka wakurugenzi na wakuu wa wilaya za mkoa huo kuhakikisha wanatenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji na kuhamasisha wageni na wazawa kujenga viwanda ili kuinua uchumi wa wananchi lakini wahakikishe wawekezaji wan je wanafuata taratibu za nchi kwa wafanyakazi kwa kuzingatia sheria za kazi.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa kiwanda hicho Yang Zhen alisema kuwa kiwanda hicho ni cha pekee kwani kitakuwa cha pili barani Afrika kwa ukubwa na cha kwanza Tanzania kwa uzalishaji wa vigae ambapo kwa siku kitakuwa kikizalisha meta 80,000 kwa siku.
Zhen alisema kuwa maradi huo una thamani ya dola za Kimarekani 100 na umegawanyika kwenye hatua mbili ambapo awamu hii ya kwanza itaisha mwishoni mwa mwaka huu huku ile ya pili ikiisha mwishoni mwa mwakani hivyo bidhaa hizo za vigae zitakuwa zikizalishwa hapahapa na siyo nje ya nchi.
Aidha alisema kuwa wanatarajia kujenga shule, kuwapatia maji, zahanati pamoja na kituo cha polisi ikiwa ni kama mchango wao kwa jamii inayozunguka kiwanda hicho ambapo mara kitakapokamilika kitaajiri watu 2,000 na kwa sasa kimetoa ajira kwa watu 200.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment