Na Mwandishi Wetu, Kibaha
WAKAZI wa Mtaa wa Muheza kata ya Maili Moja wilayani Kibaha
mkoani Pwani wamefunga ofisi ya mtaa huo kwa madai ya kuukata uongozi ambao
wamesema haufanyi kazi kwa utaratibu uliowekwa ikiwa ni pamoja na kutofungua
ofisi.
Wakizungumza na waandishi wa habari walisema kuwa uongozi huo
tangu umechaguliwa umeshindwa kabisa kuwajibika hivyo kushindwa kuleta
maendeleo kwa kipindi chote cha uongozi wao walipochaguliwa mwishoni mwa mwezi
Oktoba mwaka jana.
Moja ya wakazi hao ambaye alijitambulisha kwa jina la
Modestus Mpelembwa alisema kuwa uongozi huo chini ya mwenyekiti wake Maulid
Kipilili umeshindwa kabisa hata kuitisha mikutano ya kisheria ambayo ndiyo
sehemu ya wananchi kuweza kuchangia maendeleo na kujua kinachoendelea ndani ya
mtaa huo.
“Wananchi wamefikia hatua ya kufunga mlaango wa ofisi
kutokana na kuona kuwa hawana msaada wowote na uongozi ambapo hata kama
unashida huwezi kusaidiwa kwani hakuna kiongozi hata mmoja anayeonekana zaidi
ya kuonekana kwa matukio maalumu,” alisema Melembwa.
Mpelembwa alisema kuwa hata mapato ya mtaa hayaonekani licha
ya kuwa mtaa huo ni moja ya mitaa ambayo ina maeneo makubwa ya ardhi ambayo
yanauzwa kama viwanja kwa ajili ya makazi kutokana na eneo hilo kuanza kujengeka
kwa sasa.
“Ofisi muda mwingi imefungwa kama una shida umpigie simu
mwenyekiti na kama ni suala la mauziano ya viwanja ni huko huko na siyo ofisini
kama taratibu zinavyosema hali ambayo inaonyesha kuwa hakuna uwazi wa fedha za
asilimia zinazotakiwa kubaki kwenye mtaa kwa ajili ya shughuli za maenedeleo,”
alisema Mpelembwa.
Naye Angela Mduma alisema kuwa uongozi huo haufai kuwaongoza
kwani umeshindwa kukabili changamoto za wananchi ambao waliwachagua kwa ajili
ya kutatua kero mbalimbali ikiw ani pamoja na ubovu wa barabara.
“Tuna chanagamoto nyingi ikiwa ni pamoja na ukosefu wa
zahanati, shule ya msingi, maji pamoja na huduma nyingine za kijamii lakini
endapo uongozi ungekuwa makini kupitia mikutano kama ingekuwa inafanyika
tungeweka vipaumbele vya kuanza kuvifanyia kazi lakini uongozi hauna
ushirikiano hakuna kilichofanyika hadi sasa,” alisema Mduma.
Mduma alisema kuwa kwa upande wa kinamama wanapata taabu hasa
kwenye huduma za kiafya kliniki kwa wajawazito, kuwapeleka watoto wao kliniki
na matibabu kwa ujumla kwao ni changamoto kubwa sana.
Naye Modestus Mapunda alisema kuwa mara ya mwisho mwenyekiti
aliitisha mkutano wa mtaa lakini cha ajabu muda mfupi baadaye aliahirisha
wakati tayari wananchi wameshajiandaa kwa mkutano hali ambayo ilisababisha
wananchi kushikwa na hasira na kuifunga ofisi.
“Tunachotaka ni mkuu wa wilaya kuja hapa kwa ajili ya kujua
kero zetu kwani uongozi umeshindwa kufanya kazi lakini cha kushangaza wajumbe
kutakiwa kutofanya chochote na mwenyekiti na hawaruhusiwi kuingia ofisini hadi
watakapoitwa,” alisema Mapunda.
Mwenyekiti wa mtaa huo Maulid Kipilili alisema kuwa hawezi
kuongea chochote kwani anaongea na uongozi wa juu na pia suala hilo tayari
amelipeleka polisi kulalamika wananchi hao kufunga ofisi ya mtaa.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Maili Moja Ramadhan Lipwai
alisema kuwa kufungwa kwa ofisi hiyo ni kinyume cha utaratibu kwani ile ni mali
ya umma na wananchi wanapata huduma kupitia ofisi hiyo.
Lipwa alisema kuwa anafanya mawasiliano na viongozi
mbalimbali ili kupata suluhu la tatizo hilo ili ofisi hiyo iweze kufunguliwa
ili wananchi waweze kupata huduma kupitia ofisi hiyo ambayo imefungwa tangu Mei
15 baada ya mkutano wa mtaa kushindwa kufanyika.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment