Thursday, February 28, 2013

FRIENDS OF SIMBA WATAKIWA KUJITOKEZA KUTATUA MGOGORO



Na John Gagarini, Kibaha
MARAFIKI wa Simba (Friends of Simba) wametakiwa kuingilia kati tatizo lililopo kwenye klabu yao ili iweze kuwa na mwenendo mzuri katika mashindano mbalimbali inayoshiriki timu yao.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi msemaji wa tawi la Simba wilayani Kibaha “Simba Tishio” Fahim Lardhi alisema kuwa hadi sasa timu hiyo bado haijapata tiba ya tatizo lililopo ndani ya klabu hiyo.
Lardhi alisema kuwa wakati huu wa matatizo wanachama na wadau wa Simba lazima wajitokeze kusaidia timu ili iweze kufanya vema kwani kwa sasa mwenendo wake ni mbaya.
“Marafiki wazuri huonekana wakati wa shida hivyo tunataka marafiki wetu wajitokeze kuinusuru timu kwani kwa sasa timu inaonekana kufanya vibaya kwenye michezo yake tofauti na matarajio ya wengi,” alisema Lardhi.
Alisema kuwa marafiki wa Simba mbali ya kusaidia fedha pia wanatakiwa kuisaidia timu hiyo kwa mchango wa mawazo ili kujua tatizo lililopo hadi timu kufanya vibaya kwenye michezo yake.
“Wanapaswa kuonyesha upendo wao kwa klabu kwani hadi sasa hatujaona jitihada zozote walizofanya kuinusuru timu na matokeo mabaya, tunawpongeza wanaposaidia timu katika mazingira yote pia waonyeshe upendo hata kama timu inafanya vibaya ili kuinusuru timu yetu ambayo inatetea ubingwa wake wa ligi kuu ya Tanzania Bara,” alisema Lardhi.
Msemaji huyo wa tawi la Simba wilayani Kibaha alisema kuwa Wanasimba wanatakiwa kuungana katika kipindi hichi kigumu kinachoikabili timu yao kwa kuwa na matokeo mabaya inayoyapata ili kujinusuru na kupata matokeo mazuri.
“Tunapaswa kuungana na kuonyesha mshikamano ili kuisaidia timu yetu kwani timu inapofanya vibaya tunaumia sana hivyo tuungane ili kuiletea maendeleo mazuri,” alisema Lardhi.
Ameipongeza kamati ya utendaji kwa kuandaa mkutano wa kujadili kiini cha timu kufanya vibaya katika michezo yake hali ambayo inaifanya timu hiyo kuwa kwenye mashaka ya kutetea ubingwa wake.
Mwisho.    

No comments:

Post a Comment