Na Mwandishi
Wetu, Kibaha
SAKATA la kugombea
mipaka kwa wakazi wawili wa Mtaa wa Visiga Kati wilayani Kibaha mkoani Pwani
limechukua sura mpya baada ya mlalamikiwa kuwasweka walalamikaji rumande licha
ya licha ya baraza la ardhi la mtaa huo kutoa maamuzi.
Maamuzi ya
baraza hilo yalitoa maamuzi kuwa mlalamikiwa Bw Salum Mnjovu asogeze mpaka huo
ambao ulileta mzozo baina yake na jirani yake Bw Henrik Simbanyamba.
Hata hivyo baada ya maamuzi hayo Bw Simbanyamba
alilalamika kuwa yeye na Bw Ally Mnola na Bi Ashura Mohamed walikamatwa na
polisi baada ya Bw Mnjovu kwenda polisi kulalamika kuwa wameharibu mali zake.
Alisema kuwa
anashangaa kukamatwa kwani shauri lilisha amuliwa na baraza na hata kama ana
malalamiko ilipaswa aende mahakama ya juu kwenda kutoa mamalamiko yake.
Alisema walikamatwa
na askari wa kituo cha polisi Visiga na kushikiliwa kwa muda kabla ya kuachiwa
nakuwa nje kwa dhamana hadi Jumanne ambapo suala hilo litaendelea.
“Tunachotaka
sheria zifuatwe kwani sisi majirani zake tuna kosa gani hadi tunakamatwa kwani
kama ni maamuzi yalitolewa na baraza likaweka mipaka halali,” alisema Bw
Simbanyamba.
Bw Mnjovu
alitakiwa arekebishe mpaka lakini alipingana na maamuzi hayo kwa kusema kuwa
yeye alipouziwa na Bw Seko Mbaruku alionyeshwa tofauti na anashangaa kwanini
asogeze mpaka ambapo alilalamika kuwa ameweka kisima cha chini hivyo itabidi
kibomolewe.
“Mimi
sikubaliani na maamuzi yaliyotolewa kwani wakati nanunua eneo hili kwa thamani
ya shilingi milioni 5 toka kwa Bw Mbaruku nilionyeshwa mipaka mbele ya uongozi
wa mtaa akiwemo mwenyekiti Bw Hemed Mpaki na ofisa Mtendaji wa mtaa Bw Benedict
Maganga nashangaa leo kuambiwa kuwa mpaka umekosewa,” alisema Bw Mnjovu.
Alisema kuwa
anashangaa kuona maamuzi yanatolewa huku viongozi wa mtaa hawapo ambao ndiyo
walikuwepo wakati wa mauziano na mipaka ilipokuwa inaonyeshwa walikuwepo.
“Sijaridhika
na maamuzi nitakwenda mbele ili niweze kupata haki yangu kwani naona haki
haijatendeka kwa upande wangu niko hapa miaka miwili iliyopita hakukuwa na
maneno, pia mawe niliyoweka niliweka kwenye mpaka wangu na sikuingia kwenye
eneo la mtu,” alisema Bw Mnjovu.
Naye mlalamikaji
Bw Simbanyamba alisema kuwa alishangaa kuona jirani yake akingoa michungwa
ambayo ndiyo iliyokuwa mipaka kasha kuweka mawe ndani ya eneo lake jambo ambalo
lilimfanya aende kwenye baraza kutafuta haki yake.
“Miezi miwili
iliyopita tuliona anaweka mawe na tulivyojaribu kumwambia kuwa mipaka hiyo ni
ya asili hivyo asiitoe lakini alingoa michungwa na mnazi kisha kusogeza mpaka,”
alisema Bw Simbanyamba.
Kaimu mwenyekiti
wa baraza hilo Bi Mwanahawa Husein alisema kuwa baraza hilo limefuata sheria na
halijamuonea mtu kwani lenyewe linatenda haki na kama mlalamikiwa anaona
kaonewa anaruhusiwa kukata rufaa ndani ya siku 45.
Kwa upande
wake mwenyekiti wa mtaa huo Bw Hemed Mpaki alisema kuwa mipaka ilikuwa ni
michungwa ambapo wakati wa mauziano mlalamikaji Bw Simbanyamba hakuwepo.
“Muuzaji Bw
Mbaruku alimwelekeza vibaya mipaka na suala la kupanda mawe ilibidi majirani
wote wawepo ili kuondoa migogoro jambo ambalo majirani hawakushierikishwa,”
alisema Bw Mpaki.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment