Na John Gagarini, Kibaha
NYUMBA ya mwenyekiti wa mtaa waPicha ya Ndege wilayani Kibaha
mkoani Pwani imeungua moto ambapo watoto wawili wadogo waliokuwa wamelala
wamenusurika kufa baada ya kuamka muda mchache kabla ya tukio la moto.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mwenyekiti
huyo Bw Godfrey Mwaipopo alisema kuwa moto huo ulitokea majira ya saa 9 alasiri
ambapo kulikuwa hakuna mtu na nyumba ikiwa imefungwa kabla ya majirani
kujitokeza na kuzima moto huo.
Bw Mwaipopo alisema kuwa watoto hao Ibrahim Hausi (2) mjukuu
wake na Olebu Lugano mwaka mmoja na nusu ambaye ni mtoto wa shemeji yake walikuwa
wamelala kama kawaida kwani mara baada ya kula ni kawaida kutakiwa kulala
walilala ambapo kwa bahati nzuri waliamka na kwenda kucheza.
“Tunamshukuru Mungu kwani wakati moto huo unatokea watoto
wale walisha amka na kwenda kucheza kwani kulikuwa hakuna mtu mzima mimi
nilikuwa kwenye kikao Halmashauri ya Mji na mke wangu alikwenda kwenye masuala
ya mikopo lakini ghafla nilipigiwa simu na jirani na kuambiwa kuwa nyumba yangu
inawaka moto,” alisema Bw Mwaipopo.
Alisema alipofika alikuta majirani wakiwa wamejaa na kufanya
jitihada baada ya kuvunja milango na kuanza kuzima moto huo ambao ulianzia
kwenye swichi ya umeme, na kuzima moto huo ambao ulianza kusambaa kwa kasi.
“Kwa kweli hakuna mtu aliyejeruhiwa na moto huo licha ya vitu
kadhaa kuungua ikiwemo vyeti, nguo makochi na kitanda na cha kushangaza ni
kwamba eneo hili lina tatizo la maji lakini maji yalipatikana kwani kila mtu
alichukua akiba na kuja kuuzima moto pia walitumia mchanga,” alisema Bw
Mwaipopo.
Aidha alisema kuwa gari la zima moto lilifika lakini walikuta
moto umeshazimwa na lilichelewa kutokana na miundombinu kutoruhusu kupita hivyo
walitumia muda mwingi kutafuta njia ya kupita.
Aliwashukuru sana wananchi wa mtaa huo kwa kujitokeza kwa
wingi kwa kutoa msaada wa kuzima moto huo vinginevyo nyumba hiyo ingeteketea
yote na kusingeweza kuokolewa kitu.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
ASKARI wa usalama barabarani mkoani Pwani wametakiwa kuongeza
juhudi katika kuzuia ajali za magari barabarani ambapo kwa mwaka jana mkoa huo
uliongoza kwa kupunguza ajali hapa nchini.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki mjini Kibaha na aliyewahi
kuwa kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani Ernest Mangu wakati wa sherehe ya kumwaga
ambapo amehamishiwa mkoa wa Mwanza na kumkaribisha kamanda mpya Ulrich Matei.
Kamanda Mangu alisema kuwa kwa kipindi cha mwaka mmoja na
miezi mitano aliyokaa kwenye mkoa huo kwa kushirikiana na askari wengine
walifanikiwa kupunguza ajali ambapo mkoa uliongoza na kuwa wakwanza.
“Mkoa wa Pwani ulikuwa ni moja ya mikoa iliyokuwa ikiongoza
kwa kuwa na ajali nyingi za magari hasa ikizingatiwa kuwa mkoa huo ndiyo lango
kuu la kuingilia Jiji la Dar es Salaam kutoka mikoani na nje ya nchi,” alisema
Kamanda Mangu.
Alisema kuwa kikubwa kilichosababisha mkoa kufanikiwa kupunguza
ajali za magari ni kutokana na ushirikiano baina ya askari wa usalama
barabarani na wadau wengine ikiwemo kamati ya usalama barabarani ya mkoa.
“Nawaomba mumpe ushirikiano kamanda mpya ili muendeleze
rekodi ambayo mliiweka mwaka jana kwa kufanya kazi nzuri ya kuzuia ajali
barabarani ambazo zimekatisha maisha ya watu na wengine kuwa na ulemavu,”
alisema Kamanda Mangu.
Kwa upande wake kamanda Matei alisema kuwa kwa kushirikiana
na wenzake watafuata nyayo za mwenzake ili kuhakikisha mkoa unakuwa mbele
kupambana na ajali.
“Mbali ya kuongoza kwa kupunguza ajali pia mkoa ulifanikiwa
kuongoza kwa kukusanya fedha kutokana na makosa mbalimbali ya barabarani na
kuushinda hata mkoa kama Mwanza amabo ni Jiji,” alisema Kamanda Matei.
Kamanda Matei alisema kuwa anaomba ushirikiano toka kwa
wananchi wa mkoa huo ili waweze kukabiliana na maovu mbalimbali kwenye mkoa huo,
sherehe hiyo ilihudhuriwa na viongozi waandamizi wa jeshi hilo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment