Thursday, February 28, 2013

KAYA ZAIDI YA 1000 ZAKUMWA NA NJAA



Na John Gagarini, Bagamoyo
KAYA 1,138 katika vijiji vitano kwenye kata ya Miono wilayani Bagamoyo mkoani Pwani vinakabiliwa na baa la njaa na kuhitaji msaada wa chakula.
 Kwa mujibu wa Diwani wa kata hiyo Sangali Kiselu alisema kuwa kaya hizo zinahitaji msaada ili kukabiliana na njaa hiyo.
Kiselu alisema kuwa kutokana na tatizo hilo uongozi wa kata ya Miono umeiomba serikali Mkoani Pwani  kuharakisha kuwapatia msaada wa chakula kaya hizo ili kukabiliana na tatizo hilo.
“Hali kwa sasa inazidi kuwa mbaya katika kaya hizo ikiwa ni kati ya kaya 4,271 zenye watu zaidi ya 20,000 ambazo zimekumbwa na baa hilo la njaa,” alisema Kiselu.

Alivitaja vijiji ambavyo vimepata athari hiyo kuwa ni
Kweikonje, Masimbani, Mihuga, Kikalo na Miono kwenye kata hiyo.

Kwa upande wake mtendaji wa kata hiyo Ramadhani Nguya alisema kwa sasa wanahofia kutokana na hali kufikia pabaya hivyo haina budi kutoa kilio hicho kwa niaba ya wananchi ili kunusuru maisha yao.

Naye Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Ahmed Kipozi amekiri kuwepo kwa hali hiyo nakusema si kweli kuwa serikali inachelewesha kupeleka msaada wa chakula katika maeneo hayo.

“Serikali imeshaidhinisha tani 400 ambazo zitasambazwa katika maeneo mbalimbali yaliokumbwa na baa hilo wilayani humo, ikiwa ni pamoja na kata ya Kibindu, Mbwewe, Kimange, Miono na Kiwangwa ambayo haijapata athari sana.

Kipozi alisema kuwa janga la njaa limezikumba kata hizo kutokana na mavuno hafifu kwa mwaka jana yaliyosababishwa na mvua iliyokuwa hairidhishi hivyo kwa sasa amehimiza kilimo cha mhogo na mtama ambayo yanahimili ukame.

Mwisho

No comments:

Post a Comment