Na John Gagarini, Kibaha
MWANAFUNZI wa darasa la kwanza wa shule ya Msingi Mbaya, Geuza Patrick (12)
amekufa kwa kujinyonga kwa kamba ya katani.
Kwa mujibu wa kaimu kamanda wa Polisi mkoani Pwani Gregory
Mushi alisema kuwa tukio hilo
lilitokea Februari 13 mwaka huu majira ya saa 12 jioni huko kitongoji cha
Msufini tarafa ya Chalinze wilayani Bagamoyo.
Bw Mushi alisema kuwa mwanafunzi huyo alijinyonga kwenye Mti
wa Mwembe nyumbani kwao.
Alisema kuwa chanzo cha kujinyonga bado hakijafahamika na
polisi wanaendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo.
Aidha alisema mwili wa marehemu ulikabidhiwa kwa ndugu kwa
ajili ya mazishi.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
SHULE ya Sekondari ya Bundikani ya Kata ya Maili Moja
wilayani Kibaha imeanza kuchukua hatua kali kwa wanafunzi wanaovaa suruali za
kubana maarufu kama modo kwa kuzichana.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha mwalimu
mkuu wa shule hiyo Bi Flora Chibululu alisema kuwa juzi walichana suruali za
wanafunzi watatu kutokana na kwenda shuleni na suruali hizo kinyume cha sheria.
Alisema kuwa baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo wamekuwa na
tabia ya kuzirekebisha kwa kuzibana
suruali hizo licha ya kuwa zinashonwa kawaida na kukiuka taratibu za shule.
“Suruali hizo za shule hushonwa vizuri lakini wao huzipeleka
kwa fundi na kuzibana sawa na miili yao maarufu kama modo, tulishawapiga marufuku kuzibadili nguo hizo
lakini wanakaidi hali iliyotufanya tuchukue hatua hiyo ili kuleta nidhamu
shuleni,” alisema Bi Chibululu.
Bi Chibululu alisema kuwa baadhi ya wanafunzi wamekuwa
wakikiuka taratibu za shuleni na kuiga tabia ambazo zinashusha taaluma hivyo
shule itakabiliana na vitendo kinyume cha taratibu za shule.
Aidha alisema wataendelea kuzichana suruali hizo kwa
mwanafunzi atakaye vaa kinyume cha sheria za shule kwani huo ni utovu wa
nidhamu na lazima wanafunzi wafuate taratibu za shule.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
AKINA Mama Lishe na Baba Lishe kwenye kata ya Maili Moja
wilayani Kibaha mkoani Pwani wametakiwa kupima afya zao kwa mujibu wa sheria
ili waweze kuhudumia wateja wao wakiwa na afya njema vinginevyo watapelekwa
mahakamani kwa kukiuka kanuni za afya.
Hayo yalisemwa na ofisa afya wa kata hiyo Bw Ally Shah,
wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha na kusema
kuwa watakao kataa kupima afya watapelekwa mahakamani.
Bw Shah alisema kuwa hivi karibuni baadhi ya wahusika
waligoma kwenda kupima afya zao wakidai kuwa kiwango cha kupima ambayo ni
shilingi 5,000 ambayo ilipangwa na halmashauri kuwa ni kubwa.
“Makundi hayo yanatakiwa kupima afya ili kutoa huduma wakiwa
na afya njema ili kuepuka maambukizi ya magonjwa mbalimbali kama
vile kifua kikuu na magonjwa ambayo yanaambukizwa kwa haraka,” alisema Bw Shah.
Alisema kuwa baadhi ya wafanyabiashara hao wamekuwa na hofu
ya kupima afya kuwa wataonekana na maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI jambo ambalo
alisema kuwa upimaji huo hauhusiani na kupima vipimo vya ugonjwa huo.
“Wasihofie kupima afya kwani magonjwa yanayopimwa hayahusiani
na ugonjwa huo na kama mtu anataka kupima ugonjwa huo ni hiyari yao wenyewe na si kwa lazima kama
sheria inavyoelekeza,” alisema Bw Shah.
Aidha alisema kuwa magonjwa yanayopimwa ni pamoja na magonjwa
ya zinaa, kifua kikuu na haja kubwa hivyo wafanyabiashara wapime kwani ni kwa
faida yao na
wateja wanaowahudumia.
Katika hatua nyingine alisema kwa sasa wanaendelea na
kuboresha usafi wa mazingira ambapo vimeundwa vikundi mbalimbali vya usafi kwa
ajili ya kuhakikisha mazingira ya Mji wa Kibaha ambapo sheria ndogondogo ya
halmashauri inawatoza kiasi cha shilingi 50,000 kwa mtu atakayetupa uchafu
kiholela.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment