Na Mwandishi Wetu, Kibaha
SAKATA la kutafuta wanafunzi watoro katika shule ya
Sekondari ya Bundikani Kata ya Maili Moja wilayani Kibaha limeibua mapya baada
ya mwanafunzi wa kidato cha pili kukutwa kwa kwa mwanaume ambaye ni kinyozi
baada ya kushindwa kwenda shule kwa muda wa siku tatu.
Mwanafunzi huyo ambaye ni miongoni mwa wanafunzi waliofeli
mtihani wa kidato cha pili mwaka jana na kutakiwa kurudia kidato cha pili mwaka
huu, alikutwa kwa kijana huyo Martin Joseph (16) mkazi wa Maili Moja shuleni
jirani na shule hiyo.
Tukio hilo lilitokea juzi baada ya kijana huyo kukamatwa na
mgambo wa kata ambao wamepewa kazi ya kuwakamata wanafunzi watoro wa shule hiyo
ambapo hivi karibuni baadhi ya wanafunzi walikamatwa porini huku wengine wakiwa
na kondomu na kupewa adhabu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuchapwa viboko na
wazazi wao kwenye baraza la kata hiyo.
Kijana huyo alifikishwa kwenye baraza la usuluhishi la kata
ya Maili Moja linaloongozwa na
mwenyekiti Bw Amadeus Ngombale, aliskiri kukaa na mwanafunzi huyo kwa kipindi
hicho licha ya kuwa mwanafunzi huyo kutokwenda shule tangu ilipofunguliwa
mwanzoni mwa mwezi huu.
“Mimi sikujua kama ni mwanafunzi kwani hakuniambia anasoma
shule na nilikaa naye kwa siku tatu ila nilishangaa kuona mgambo wamekuja ofini
kwangu na kunikamata kwa madai kuwa ni kwanini nimekaa na mwanafunzi na
kumsababisha asiende shule,” alisema Joseph.
Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule hiyo Flora Chibululu
alisema kuwa mwanafunzi huyo ni moja kata ya wanafunzi wlaiofeli mwaka jana
kidato cha pili na kutakiwa kurudia kidato hicho lakini walishangaa ni kwanini
haendi shule.
“Huyu mwanafunzi ni miongoni mwa wale wanaorudia kidato cha
pili mwaka huu na baada ya kukutwa kwa mwanaume tulimpa barua aje na mlezi wake
ambaye ni bibi yake ambaye ndiye anayeishi naye,” alisema Chibululu.
Aidha alisema kuwa mwanafunzi huyo alisema kuwa anaishi na
bibi yake kwa sababu baba yake hamtunzi kutokana na tabia zake ambazo zimekuwa
ni kero.
Kijana huyo kutokana na kukubali tuhuma hizo alipelekwa
polisi kwa ajili ya kufikishwa mahakamani kutokana na tukio hilo ambalo ni moja
ya changamoto kubwa kwa wanafunzi wa kike kwenye wilaya ya Kibaha na mkoa wa
Pwani
Mwisho.
No comments:
Post a Comment