Na John Gagarini,
Kibaha
SERIKALI imewaonya wananchi wanaojichukulia sheria mkononi
kwa kuwaua watuhumiwa badala yake wawapeleke kwenye vyombo husika ili
wachukuliwe hatua za kisheria.
Hayo yalisemwa na kamanda wa polisi mkoani Pwani Ulrich Matei
ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya siku ya sheria (Law Day) na
kusema kuwa watu wengi wamepoteza maisha katika mkoa huo kutokana na watu
kujichukulia sheria mkononi.
Kamanda Matei alisema kuwa vyombo vya kutoa haki vipo hivyo
wananchi wa mkoa huo hawapaswi kuwaua watuhumiwa kwani wengine wanakuwa hawana
hatia.
“Watu wengi wameuawa na watu wanaoojiita kuwa wana hasira
kali na kuwafanyia vitendo vya kinyama watuhumiwa wa wizi wa pikipiki, kuku na
vitu vidogovidogo,serikali haitakuwa tayari kuona vitendo hivyo vinaendelea,”
alisema Kamanda Matei.
Alisema kuwa watu hao wanaojiita wenye hasira kali mbali ya
kuua watuhumiwa wameharibu miundombinu mbalimbali ya watu na serikali jambo
ambalo ni kinyume cha sheria.
“Tabia hii kwa sasa imeshamiri na kushika mizizi kwa sasa kwenye
mkoa wa Pwani jambo hili ni kinyume cha sheria na haki za binaadamu kwani hata
katiba inalinda haki ya mtu kuishi,” alisema Kamanda Matei.
Aidha alivitaka vyombo vya kutoa haki kutochelewesha kutoa
maamuzi ili kuondoa dhana kuwa haki haitendeki na kufikia watu kujichukulia
sheria mkononi.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment