Na John Gagarini, Kibaha
MWANAFUNZI wa shule ya sekondari ya Pangani Kata ya Pangani ambaye
alikuwa aingie kidato cha pili mwaka huu mwenye umri wa miaka (16) ameshindwa
kwenda shule baada ya kutekwa na vijana watatu kwa kipindi cha miezi mitatu
ambapo alipata mimba na vijana hao waliitoa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha huku
akibubujikwa na machozi alisema kuwa vijana hao ambao ni wakulima kati yao
wawili ni ndugu walimteka kwa kutumia visu walivyokuwanavyo.
Aliwataja vijana hao ambao anawatuhumu kumfanyia kitendo
hicho kuwa ni Jonas Edward, Isaka Joseph na Faida Joseph ambao ni ndugu walimteka
Novemba 3 mwaka jana baada ya kumdanganya kuwa anatakiwa kwenda kuchukua mzigo
wa ndugu yake.
“Baada ya kwenda kufuata mzigo huo niliwakuta wakiwa na visu
vitatu ambapo kila mmoja alikuwa na kisu na kunipeleka kwenye nyumba waliyokuwa
wakiishi kusema kuwa hapo ndipo nitakapokuwa naishi na endapo nitajaribu kutoka
basi wataniua,” alisema mwanafunzi huyo.
Alisema kuwa kwa kipindi chote hicho walikuwa wakifunga mlango
kwa nje kwa kutumia kufuli kwa nje hali ambayo ilimfanya ashindwe kutoka pia
ikizingatiwa kuwa nyumba hiyo iko mbali na nyumba zingine na kuwa katika
kichaka.
“Faida ambaye ndiye aliyenifanya kama mke wake alinipa mimba
lakini baada ya kuona hivyo walinilazimisha kuitoa kwa kutumia majani ya chai
ambayo yalichemshwa na maji na kuniamuru ninywe na kusababisha mimba kutoka
ambapo nilitokwa na damu nyingi na kupata maumivu makali,” alisema mwanafunzi
huyo.
Aidha alisema kuwa walimtengenezea kajumba kadogo kwa kupanga
matofali na miti kisha yeye kuingia humo mfano wa kaburi ambapo alikuwa
akijisaidia kwenye mifuko ya plastiki na chupa kwa ajili ya haja ndogo na kuoga
ni humo ndani.
“Kwa upande wa chakula walikuwa wakipika usiku tu kwani
walikuwa wakifika majira ya saa sita au saba usiku wanapika tunakula ila
asubuhi na mchana nilikuwa sili chakula hata mavazi yangu waliyachoama moto
nikawa navaa nguo ya moja ya vijana hao,” aliongeza.
Aliongeza kuwa siku moja vijana hao walisahau kufunga mlango
na ndipo alipotoka na kuomba msaada kwa mtu ambaye alimpeleka hadi nyumbani kwa
walezi wake ambao ni babu na bibi yake ambao ndiyo waliokuwa wakiishi naye kwa
muda wote.
Kwa upande wake babu wa mwanafunzi huyo Daud Zakayo alisema
kuwa mwanafunzi huyo alitoweka katika mazingira ya kutatanisha na walifanya
jitihada kumtafuta ambapo walitoa taarifa polisi na kwa ndugu lakini bila ya
mafanikio.
Zakayo alisema kuwa baada ya mjukuu wao kupatikana walitoa
taarifa polisi ambapo vijana hao walikamatwa kwa ajili ya mahojiano kuhusiana
na tukio hilo. Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Ulrich Matei alipoulizwa
kuhusiana na tukio hilo alisema kuwa bado hajapata taarifa.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment