Na John
Gagarin, Kibaha
SHIRIKA la
ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Pwani imeanza utaratibu wa kuingia
mkataba na wadeni wake kwa kuwaondolea riba ya madeni yao katika kipindi cha
Januari hadi Juni mwaka huu.
Akizungumza na
waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha meneja wa TANESCO mkoa huo Bw
Jonson Mwigune, alisema kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuwapunguzia mzigo
wateja wao.
Bw Mwigune
alisema kuwa mbali ya kuwaondolea riba ya madeni yao kwa kipindi hicho pia
watakuwa wakilipa kidogo kidogo hadi watakapomaliza madeni.
“Mkataba huo
utawawezesha wateja wetu kupata nafuu ya madeni pia atarejeshewa umeme huku
akiendelea kulipa kidogokidogo tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo mteja
alikatiwa umeme hadi atakapomaliza deni lake,” alisema Mwigune.
Alisema kuwa
kwa sasa shirika liko kwenye mkakati wa kupunguza madeni kwa wateja wao ambapo
moja ni kuingia mikataba na wateja wao ili waonyeshe jinsi gani watakavyolipa
huku wakiendelea kupata huduma.
“Mkakati
mwingine wa kupunguza madeni ni kuweka Luku ambapo kwa sasa asilimia zaidi ya
95 wameshaunganishwa kwenye mfumo huo ambao mteja hulipia kadiri anavyotumia,”
alisema Bw Mwigune.
Aidha alisema
mkakati ni wateja wote kutumia Luku ambapo Wizara ya Nishati na Madini
imepunguza gharama za umeme kwa asilima 30 ili wananchi wengi waweze kuwa na
umeme huku mkoa ukiwa na mpango wa kuwafikia wateja 17,500.
Aliwataka wananchi
kushirikiana na shirika hilo kulinda miundombinu ikiwa ni pamoja na nyaya, mafuta
na mafuta yake ili kutosababisha umeme kukatika
Mwisho.
No comments:
Post a Comment