Na John Gagarini, Kibaha
DIWANI wa kata ya Maili Moja Bw Andrew Lugano
amesikitishwa na mamalaka ya maji safi na majitaka (DAWASCO) kushindwa
kuwahudumia wananchi hali inayosababisha kukosa maji kwa zaidi ya mwezi sasa.
Akizungumza mara baad aya kufanya ziara kwenye kata
hiyo kuangalia maeneo ambayo yamekuwa yakikosa maji kwa muda mrefu, huku akiwa
ameambatana na meneja wa DAWASCO Bw Robert Mugabe alisema kuwa hakuna sababu ya
wananchi kukosa maji kwa muda wote huo na uongozi upo.
Bw Lugano alisema kuwa amekuwa akipata kero hiyo ya
maji toka kwa wananchi na jitihada zake za kufuatilia zimekuwa zikigonga mwamba
hali iliyomlazimu kumtoa meneja huyo ofisini kwake Jumamosi na kumwonyesha
jinsi gani wananchi wanavyotaabika kwa kukosa maji.
“Siwezi kukubali kuona wananchi wakihangaika kutafuta
maji huku chanzo cha maji kikiwa jirani hivyo lazima kampuni hiyo ijali
wananchi ili waondokane na kero hiyo,” alisema Bw Lugano.
Moja ya wakazi wa kata hiyo ambaye anakaa mtaa wa
Mzimuni Bw Mohamed Atiki alisema kuwa wamekuwa wakipata tabu kubwa ya kupata
maji hali inayowasababisha kununua maji kwa bei ya shilingi 500 kwa dumu la
lita 20.
“Tumekuwa tukihangaika kwa kipindi kirefu licha ya
kutoa taarifa ya ukosefu wa maji kwenye kampuni hii ya maji hivyo lazima
wabadili utendaji kazi wao,” alisema Bw Atiki.
Kwa upande wake meneja wa DAWASCO Kibaha Bw Robert
Mugabe alisema kuwa tatizo kubwa lililosababisha wananchi kukosa maji ni kutokana
na ujenzi wa barabara katika kata hiyo.
“Mabomba mengi yamekatwa kutokana na ujenzi wa
barabara lakini hata hivyo tayari tumewasiliana na mkandarasi ili kuangalia
namana ya kuweza kurekebisha hali hiyo,” alisema Bw Mugabe.
Bw Mugabe alisema kuwa tayari wameshafanya tathmini ya
uharibifu uliofanyika na wakati wowote wataanza kufunga mabomba yaliyokatwa ili
wananchi hao waendelee kupata maji kama kawaida.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment