Thursday, February 14, 2013

TANESCO KUONDOA RIBA KWA WATEJA WENYE MADENI


Na John Gagarin, Kibaha
SHIRIKA la ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Pwani imeanza utaratibu wa kuingia mkataba na wadeni wake kwa kuwaondolea riba ya madeni yao katika kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha meneja wa TANESCO mkoa huo Bw Jonson Mwigune, alisema kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuwapunguzia mzigo wateja wao.
Bw Mwigune alisema kuwa mbali ya kuwaondolea riba ya madeni yao kwa kipindi hicho pia watakuwa wakilipa kidogo kidogo hadi watakapomaliza madeni.
“Mkataba huo utawawezesha wateja wetu kupata nafuu ya madeni pia atarejeshewa umeme huku akiendelea kulipa kidogokidogo tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo mteja alikatiwa umeme hadi atakapomaliza deni lake,” alisema Mwigune.
Alisema kuwa kwa sasa shirika liko kwenye mkakati wa kupunguza madeni kwa wateja wao ambapo moja ni kuingia mikataba na wateja wao ili waonyeshe jinsi gani watakavyolipa huku wakiendelea kupata huduma.
“Mkakati mwingine wa kupunguza madeni ni kuweka Luku ambapo kwa sasa asilimia zaidi ya 95 wameshaunganishwa kwenye mfumo huo ambao mteja hulipia kadiri anavyotumia,” alisema Bw Mwigune.
Aidha alisema mkakati ni wateja wote kutumia Luku ambapo Wizara ya Nishati na Madini imepunguza gharama za umeme kwa asilima 30 ili wananchi wengi waweze kuwa na umeme huku mkoa ukiwa na mpango wa kuwafikia wateja 17,500.
Aliwataka wananchi kushirikiana na shirika hilo kulinda miundombinu ikiwa ni pamoja na nyaya, mafuta na mafuta yake ili kutosababisha umeme kukatika
Mwisho.     

No comments:

Post a Comment