Na John Gagarini, Kibaha
WAKALA wa Huduma za Misitu
Tanzania (TFS) Kanda ya Mashariki wametakiwa kutoa elimu zaidi kwa wananchi juu
ya upandaji miti kuliko kuvuna ili kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi
ambayo yanapelekea uoto wa asili kutoweka.
Hayo yalisemwa jana mjini Kibaha
na Katibu Tawala mkoa wa Pwani Bi Betha Swai wakati akifungua mkutano wa wataalamu
wa sekta ya misitu kuweka mikakati mbalimbali juu ya kuboresha misitu kwenye
mkoa huo.
Bi Swai alisema kuwa ukatiji wa
miti ni mkubwa tofauti na miti inayopandwa jambo ambalo litaipelekea nchi
kukumbwa na majanga yanayotokana na uharibifu wa mazingira ikiwemo ukame,
mmomonyoko wa ardhi na ukosefu wa vyanzo vya maji.
“Ni vema mkatoa elimu kwa
wananchi kwa kiwango kikubwa ili wananchi wakawa na uelewa juu ya uharibifu wa
mazingira na umuhimu wa kutunza misitu kwani wengi wao hawaoni umuhimu wake
licha ya kuwa wanatumia zao la miti katika kujipatia kipato,” alisema Bi Swai.
Aidha alisema kuwa halmashauri na
serikali nazo zijikite kwenye utoaji elimu hiyo na si kutaka tu ushuru huku misitu ikiendelea kuteketea huku mikakati ya
kupanda miti ikiwa si mizuri.
“Tuachane
na kusema kuwa tumegawa miti sehemu Fulani kwa ajili ya kupanda kwa sasa tuwe
na mkakati wa kupanda baadhi ya maeneo mfano kwenye mabonde au sehemu ambako
kumefanyika uharibifu mkubwa ili tuonyeshe na si kusema kwa maneno tu,” alisema
Bi Swai.
Kwa
upande wake Bakari Mohamed alisema kuwa lengo la kuanzishwa wakala hao amabo ni wapya
ni kwa ajili ya kuondoa urasimu na mfumo wa kiutendaji katika utekelezaji wa
majukumu ya misitu ili kuleta ufanisi.
Bw Mohamed alisema kuwa moja ya
kazi za wakala ni kuihamasisha jamii kuanzisha misitu yao na kuilinda ile iliyopo pia kuwa na
vikundi vya uzalishaji nyuki kwa kutumia rasilimali ya misitu.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment