Wednesday, February 6, 2013

WATAKA MAJAJI WAFANYIWE USAILI



Na John Gagarini, Kibaha
SEIKALI imeshauriwa kubadili mfumo wa upatikanaji wa majaji kwa kufanyiwa usaili badala ya kuteuliwa ili kuleta utawala bora wa kisheria.
Hayo yalisemwa jana mjini Kibaha na mwakilishi wa mawakili mkoani Pwani, Saiwelo Kumwenda, wakati wa maadhimisho ya siku ya sheria nchini kwenye mkoa huo zilizofanyika kwenye viwanja vya mahakama.
Alisema kuwa ili kuimarisha utawala wa sheria ni vema waajiriwe kwa kwa kufanyiwa usaili rasmi na chombo kisicho na mfungamano wa kiutawala na serikali.
“Ni vema majaji wakaomba kazi na kufanyiwa usaili na wale watakaofuzu vigezo vinavyotakiwa ndiyo watakaopata nafasi hiyo tofauti na sasa ambapo huteuliwa na Raisi,” alisema Bw Kumwenda.
Alisema kuwa mfumo wa kuteua si mzuri katika mfumo wa kutaka kuimarisha utawala wa sheria ili kuepuka malalamiko na manunguniko.
Aidha alitaka viongozi wan chi kusaidia kulinda uhuru wa mahakama ili nchi iendelee kufuata utawala wa sheria na mfumo mzima wa demokrasia.
Pia kuchukua hatua ya kinidhamu kwa watumishi wale ambao wanaonekana au watathibitika kuwa kazi zao za kutafsiri sheria, kusikiliza mashauri na kuyatolea maamuzi hawaijui vizuri wala hawazielewi.
Kwa upande wake hakimu mkazi mfawidhi wilaya ya Kibaha mkoani Pwani Bi Bahati Ndesarua alisema kuwa utawala wa sheria una umuhimu kwa kugawa madaraka kwa kuzingatia taratibu.
Bi Ndesarua alisema kuwa utawala wa sheria unasaidia kukua kwa uchumi na watu kupata haki zao bila ya kumwonea mtu kutokana na uwezo wake.
Aliwataka wananchi kushiriki katiba zoezi la uboreshaji wa katiba mpya ili kutoa mchango wao wa mawazo na kuifanya iweze kuwa na manufaa kwa kila mtu.
Naye mgeni rasmi kamanda wa polisi mkoani Pwani Bw Ulrich Matei alisema kuwa wananchi waachane na tabia ya kuvunja sheria kwa kuwapiga na kuwaua watuhumiwa.
Bw Matei alsiema kuwa ni vema wananchi hao wakawapeleka kwenye vyombo vya sheria ili haki iweze kutendeka na si kutumia mabavu kwa kuwaua.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment