Friday, February 22, 2013


Na Mwandishi Wetu, Kibaha
ASKARI wa Jeshi la Polisi kituo kidogo Cha Kwa Mathiasi Wilyani Kibaha mkoani Pwani Pc Ramadhan amelazwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili baada ya kujeruhiwa na wananchi waliovamia kituo hicho kutaka kuwatoa watu waliowatuhumu kuwa wameiba simu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake kamanda wa polisi mkoani humo Ulrich Matei alisema kuwa tukio hilo lilitokea Februari 21 mwaka huu majira ya saa 1 usiku baada ya wananchi hao kutaka kuwatoa watu waliodai kuwa wameiba simu na kutaka kuwaua.
Kamanda Matei alisema kuwa chanzo cha tukio hilo kilianza kwenye uwanja wa mpira wa miguu baina ya timu za Palasupalasu na Kigogo ya Jijini Dar es Salaam, ambapo mchezo huo uliokuwa ukichezwa kwenye uwanja wa Mwendapole kulivunjika kutokana na vurugu zilizojitokeza.
“Baada ya mchezo huo kuvunjika washabiki wa timu hizo walianza kushambuliana na ndipo watu waliotuhumiwa ambao ni Michael Mathias (30) na Hashim Noah (19) ambaye ni mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Mwanagati Jijini Dar es Salaam kukimbia kwa kutumia pikipiki na walipoona wmezidiwa waliiacha pikipiki kisha kuingia kwenye msikiti wa Tanita,” alisema Kamanda Matei.
Aidha alisema kuwa baada ya kuingia ndani ya msikiti huo wananchi hao waliuzunguka msikiti huo kisha kutaka kuwatoa watu hao ili wawaue ndipo polisi walipofika na kuwatawanya wananchi hao lakini waligoma na kuanza kuwarushia mawe polisi ndipo polisi walipopiga risasi kuwatawanya wananchi hao.
“Katika vurugu hizo Maria Stamford alipigwa risasi ya ziwa na Idd Shukuru alipigwa mguu wa kulia kisha waliwachukuwa watu hao na pikipiki yao ndipo wanannchi hao walikwenda hadi kwenye kituo hicho wakidhani kuwa watu hao wako pale kwani waliiona ile pikipiki nje ya kituo hicho,” alisema KamandaMatei.
Aliendelea kusema kuwa walikivamia kituo hicho na kumpiga askari huyo ambaye alikuwa amevaa sare na askari mwingine Bonventura kisha kuvunja mlango na kuwaangalia watu wale lakini hawakuwakuta na kuharibu vitu mbalimbali.
“Uchunguzi ulibaini kuwa watu wale hawakuwa wezi bali walikuwa ni mashabiki wa timu mojawapo ambao walizushiwa kuwa wezi jambo ambalo si la kweli majeruhi wanaendelea vyema na matibabu na kwa sasa tayari wameunda tume ndogo kufuatilia tukio hilo na hakuna mtu aliyekamtwa kuhusiana na tukio hilo,” alisema Kamanda Matei .
Mwisho. 
  

No comments:

Post a Comment