Na Mwandishi Wetu, Kibaha
WATU nane wamefariki dunia na
wengine wawili wamejeruhiwa baada ya magari mawili kugongana uso kwa uso katika
Kitongoji cha Kibiki Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Akizungumza na waandishi wa
habari kamanda wa Polisi mkoani humo Ulrich Matei alisema kuwa kati ya watu
waliokufa wanafunzi ni wanne.
Kamanda Matei alisema kuwa
tukio hilo lilitokea Februari 11 majira ya jioni na kuyahusisha magari T363 AZG
aina ya Toyota Mark II likitokea mkoani Tanga kwenda Morogoro likiendeshwa na
Bw Abuu Ahmed na kugonagana na gari namba T 433 AYQ aina ya Mitsubishi Fuso
likitoka Morogoro kwenda Dar es Salaam likiendeshwa na Bw Mweta Daniel.
“Chanzo cha ajali hiyo
ni mwendo kasi wa dereva wa Toyota Mark II ambaye alipoteza mwelekeo baada ya
kujaribu kulipita gari lililokuwa mbele yake kisha kugongana uso kwa uso na
Fuso lililokuwa likitokea mbele na kusababisha vifo hivyo,” alisema Kamanda
Matei.
Kamanda Matei aliwataja waliokufa
kuwa ni Esaau Enos (16) aliyekuwa kidato cha tatu, Bahati Mbene (18) kidato cha nne, Latifa Shabani (17) kidato
cha nne na Stella Kazimoto (18) wote wanafunzi wa shule ya Sekondari Chalinze.
“Wengine ni Maria Lelela na
mtoto wake Samweli Ismail kati ya miaka mitatu au minne, Hassan
Kalunga na Abuu Ahmed dereva wa gari dogo,” alisema Kamanda Matei.
Aidha alisema kuwa majeruhi
ni William Tobias na Ahmada Juma aliyekuwa utingo wa fuso ambapo dereva
wa Fuso anashikiliwa na Jeshi la polisi kwa uchunguzi zaidi.
Alitoa wito kwa madereva
kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani ili kuepusha ajali na kudai kuwa
Jeshi hilo halitowavumilia madereva wazembe kwa kuwakamata na kuwachukuliwa
hatua kali wote watakaoshindwa kutii sheria za usalama barabarani.
MWISHO
No comments:
Post a Comment