Tuesday, February 26, 2013

AKUTWA AMEFIA GESTI

Na John Gagarini, Kibaha
MFANYABIASHARA wa Jijini Dar es Salaam Ambrose Mapunda mwenye umri kati ya 50 na 55 amekutwa amekufa na mwili wake kuwekwa chini ya uvungu wa kitanda wa nyumba ya kulala wageni ya Cham Cham Msata wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha kwa niaba ya kamanda wa polisi mkoa wa Pwani ofisa upelelezi wa Jeshi la polisi Juma Yusuph alisema kuwa mwili wa marehemu ulikutwa ukiwa uchi.
Kamanda Yusuph alisema kuwa tukio hilo lilitokea kati ya Fabruari 22 na 24 mwaka huu kwenye nyumba ya kulala wageni ya Cham Cham huku ukiwa na jeraha kubwa kichwani huku shingo yake ikiwa imenyongwa.
“Marehemu alikutwa akiwa chini ya uvungu huku mwili wake ukiwa hauna nguo na jeraha huku ukiwa umenyongwa shingo ambapo mtu aliyehusika na tukio hilo hakuweza kufahamika mara moja,” alisema kamanda Yusuph.
Alisema kuwa marehemu hakukutwa na chochote licha ya kuwa alifika kwenye nyumba hiyo ya kulala wageni akiwa na begi kwenye chumba namba mbili.
“Ujumbe uliokutwa kwenye chumba hicho ulisema kuwa umenidhulumu tulikubaliana unilipe kiasi cha shilingi 20,000 lakini hujanilipa, ujumbe huu umeandaikwa na mtu asiyefahamika,” alisema Kamanda Yusuph.
Aidha alisema kuwa mhuduma na mlinzi wa nyumba hiyo ya kulala wageni wanashikiliwa kwa mahojiano zaidi kuhusu tukio hilo na polisi wanaendelea na uchunguzi.
Mwisho.  

No comments:

Post a Comment