Friday, March 1, 2013

MBUNGE ALIPA HASARA ILIYOSABABISHWA NA MGAMBO


Na John Gagarini, Kibaha
MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini mkoani Pwani Silvestry Koka amelazimika kuwalipa fedha kiasi cha shilingi 275,000 wanawake watatu wanaouza samaki baada ya mgambo wa kata ya Maili Moja kumwaga samaki wao kwa madai ya kukiuka kanuni za afya.
Koka ilibidi alipe fedha hizo kwa wafanyabiashara hao baada ya kuangua kilio mbele ya mbunge huyo wakati wa mkutano na wananchi wa Kibaha.
Alisema hayo yalikuwa makosa ya kibinaadamu yaliyofanywa na mgambo hao wakati wakitekeleza zoezi la usafi kwenye maeneo mbalimbali ya mji wa Kibaha.
“Suala la afya ni muhimu na mgambo hawa waliteleza na kujikuta wakiharibu mali za wafanyabiashara ambao wanajitafutia riziki zao huku wengine wakiwa wamekopa fedha kwa ajili ya kufanyia biashara hiyo,” alisema Koka.
Mbunge huyo alisema kuwa kuanzia sasa wafanyabiashara na mgambo hao kwa kushirikiana na ofisi ya afya ya kata kila upande kufuata kanuni na sheria ili kufanikisha suala la afya.
Kwa upande wao wakinamama hao mmoja wao aliyejitambulisha kwa jina la Riziki Said alisema kuwa mgambo hao walifika kwenye biashara yake na kusema kuwa kwakuwa hakupima afya yake na kuwamwaga samaki wake wenye thamani ya shilingi 65,000.
Naye mfanyabiashara mwingine Nuru Msangi alisema kuwa mgambo hao walichukua samaki wake wenye thamani ya shilingi 75,000 na kuzimwaga kwa madai kuwa naye hakupima afya yake.
Alisema kuwa wafanyabiashara wengi wanashindwa kupima afya zao kutokana na gharama kubwa ya kupima ya shilingi 5,000 na pia walisema wao kama wanshinikizwa kupima je kwa wateja wanaokwenda kununua mbona hawabanwi.
Mbunge huyo alizitaka pande mbili hizo kati ya idara ya afya ya kata hiyo na wafanyabiashara kuanza mahusiano mazuri upya ili kuondoa ugomvi unaojitokeza mara kwa mara pia halmashauri itoe elimu juu malipo hayo ya kupima afya ya shilingi 5,000.
Mwisho.    

No comments:

Post a Comment