Saturday, March 30, 2013

WANAKIJIJI WATAKA MAKUBALIANO

Na John Gagarini, Kibaha
WAKAZI wa Kijiji cha Gama wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wameitaka kampuni ya EcoEnergy ya Sweden inayotaka kuwekeza kilimo cha miwa kukaa pamoja ili kuingia makubaliano nao juu ya kuitumia ardhi yao  badala ya kuwatumia madalali wanaojifanya wanahusika na eneo hilo.
Wakizungumza Kijijini hapo jana kwenye mkutano wa hadhara uliaondaliwa na uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Bagamoyo.
Moja ya wakazi wa Kijiji hicho Ramadhan Alawi alisema kuwa wao wanachokitaka ni kukaa meza moja na wao na si kuwatumia watu wa kati ambao hawahusiki na kuwasemea kwani ardhi hiyo ni vema kukawa na maelewano ya namna nao watakavyonufaika.
“Sisi hatukatai wawekezaji lakini tunachokitaka wawekezaji hao waje tukae meza moja na kukubaliana namna ya jinsi na sisi tutakavyoshiriki katika uwekezaji huo na hutataki watu wa kutusemea kwani sisi wenyewe tupo,” alisema Alawi.
Kwa upande wake Salum Yusuph alisema kuwa tatizo kubwa hapa ni wananchi kutoshirikishwa katika suala zima la uwekezaji huo kwa wakazi wa Kijiji chao na hawajui wao watanufaika vipi kwani waliambiwa waondoke kwenye eneo hilo.
“Hapa tunataka sisi na EcoEnergy tukae pamoja tukubaliane hasa ikizingatiwa kuwa hapa hatuna shule, zahanati wala huduma za kijamii na tungependa tuwe kama mashamba mengine ya Mtibwa na Kagera tukae tulime miwa wao waje kununua kwetu na si kutuondoa,” alisema Yusuph.
Akizungumzia suala hilo msimamizi wa wakulima wadogo wadogo wa kampuni hiyo Ian Sherry alisema kuwa wao wana lengo la kuwekeza katika kijiji hicho kwa manufaa ya wananchi na hawana lengo baya kwani kwenye vijiji walivyowekeza kupitia mradi huo wamenufaika na kuboresha huduma za kijamii.
“Wakazi wa eneo hili wasiwe na wasiwasi kwani taratibu zinafuatwa na kama kuna matatizo mambo yote yatawekwa sawa ili kuhakikisha manufaa ya mradi huo ambao utakuwa na uwekezaji mkubwa unaofikia zaidi ya bilioni saba,” alisema Sherry.
Naye mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bagamoyo Shaibu Mtawa alisema kuwa kutokana na changamoto ya madai ya wananchi wataandaa mkutano baina ya pande zote hizo ili kuondoa tofauti zilizojitokeza.
Mtawa alisema kuwa hapa inaonekana wananchi hawajashirikishwa kikamilifu juu ya uwekezaji huo hivyo chama kitahakikisha mgogoro uliopo unamalizwa na kesi iliyo mahakamani inaondolewa ili kuleta mwafaka.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment