Na John Gagarini, Kibaha
MKUU wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahizaameiomba ofisi ya Waziri
Mkuu (TAMISEMI) kuipatia hospitali ya wilaya ya Tumbi kiasi cha shilingi
milioni 160 kwa ajili ya kukarabati chumba cha kuhifadhia maiti ambacho kiko
kwenye hali mbaya.
Aliyasema hayo hivi karibuni wakati wa ziara ya siku moja ya
Waziri wa TAMISEMI Hawa Ghasia alipotembelea Shirika la Elimu Kibaha (KEC) ambalo
linamiliki hospitali hiyo ambalo liko chini ya Wizara hiyo.
Mahiza alisema kuwa chumba hicho kiko kwenye hali mbaya kwani
kimekuwa ni kidogo na kimechakaa na hakijafanyiwa ukarabati tangu kuanzishwa
miaka ya 70.
“Waziri tunaomba utusaidie kuweza kupata fedha hizo kwani
licha ya kuwa na madeni makubwa na mahitaji ya fedha, kikubwa ni chumba hichi
ambacho kinahitaji kufanyiwa ukarabati kwani kiko kwenye hali mbaya na kinahitaji
msaada wa haraka,” alisema Mahiza.
Alisema maiti zinahitaji kuhifadhiwa katika mazingira mazuru
ili kuzienzi lakini kwa hospitali yetu hali si nzuri kwani tutakuwa
hatuzitendei haki kwa kuzitunza kwenye mazingira mabaya.
Kwa upande wake mganga mkuu wa hospitali Peter Datan alisema
kuwa tatizo la chumba hicho ni kubwa kwani kwa sasa maiti zinakaa mbili mbili
ambapo kwa utaratibu wanapaswa kukaa mwili mmoja kutokana na udogo wake.
“Kwa sasa chumba kimekuwa ni kidogo kwani maiti zimeongezeka
tofauti na zamani ambapo zilikuwa chache kwani kwa sasa maiti zinazohifadhiwa
ni 20, pia maiti nyingine zinakaa muda mrefu hasa zile ambazo zinakuwa
zimeokotwa,” alisema Dkt Datan.
Dkt Datan alisema kuwa chumba hicho kinapata mzigo mkubwa wa
maiti kutokana na baadhi ya maeneo ya mikoa kama vile Dar es Salaam, Morogoro
na Tanga kuletwa TUmbi.
Naye Mkurugenzi wa KEC Dkt Cyprian Mpemba alisema kuwa
wanakabiliwa na madeni makubwa ambayo kwa sasa yanafikia zaidi ya bilioni moja
hali ambayo ni madai ya wafanyakazi na wazabuni ambao wanatoa huduma kwao.
Kwa upande wake waziri Ghasia alisema kuwa atayafanyia kazi
maombi hayo kwa kupeleka ombi maalumu hazina ili kuweza kutatua chanagamoto
zilizopo kwenye shirika hilo la Umma ambalo lilianzishwa miaka ya 70 na nchi za
Nordic kwa ushirikiano na serikali.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment