Monday, March 25, 2013

HABARI ZA P;WANI

 Na John Gagarini, Kibaha
KAMATI za Maadili kwenye klabu za waandishi wa habari nchini zimetakiwa kutumia busara katika kuwapatanisha waandishi na wadau mara kunapotokea migongano baina yao ili kumaliza pasipo kwenda mahakamani kuepusha vyombo vya habari kutozwa faini kubwa.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na ofisa kutoka baraza la habari Tanzania (MCT) Asterius Banzi wakati wa mafunzo ya siku moja kwa kamati ya maadili ya Chama Cha Waandishi wa habari mkoani Pwani (CRPC) yaliyofanyika kwenye ofisi za chama hicho.
Banzi alisema kuwa ni vema kamati hizo zikatumia uungwana kutatua migogoro kwani endapo malalamiko hayo yatapelekwa mahakamani athari zake ni kubwa hasa kwa upande wa vyombo vya habari kupigwa faini kubwa ambazo zitasababisha vyombo hivyo kufungwa.
“Baadhi ya walalamikaji wamedai fidia kubwa kwa vyombo vya habari na kupeleka vyombo hivyo kufungwa au kuyumba na kushindwa kuhudumia wananchi kupata taarifa ikiwa ni moja ya haki zao za msingi za kikatiba,” alisema Banzi.
Aidha alisema kuwa ni vema mambo hayo yakatatuliwa kirafiki kwani endapo yakifikishwa mahakamani athari zake ni kubwa kuliko yangemalizwa kwenye kamati hizo.
Pia alivitaka baadhi ya vyombo vya habari ambavyo vinakutana na matatizo ya kuwachafua wadau wao ndani ya jamii kukubali kukaa meza moja na walalamikaji ili kufikia muafaka kwa kujenga mahusiano mazuri.Banzi alisema kuwa vyombo vya habari na wananchi ni marafiki hivyo lazima kuwe na mahusiano mazuri kwa pande zote ili kuepuka migogoro isiyo na lazima.
Katika hatua nyingine kamati hiyo imemchagua wakili wa kujitegemea Saiwelo Kumwenda kuwa mwenyekiti wa kamati hiyo ambayo imetuliwa na chama hicho.
Nafasi ya makamu mwenyekiti ilikwenda kwa Elizabeth Ngai huku katibu wa kamati hiyo akiwa ni Athuman Mtasha.
Kamati hizo kwenye klabu za waandishi wa habari ziliundwa kwa lengo la kusuluhisha migogoro baina ya wanahabari na wadau ili kuzingatia maadili ya kazi za waandishi wa habari.
Mwisho.
 
Na John Gagarini, Kibaha
MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini mkoani Pwani Silvestry Koka amewataka waandishi wa habari mkoani humo kujiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwenye kambi ya Ruvu uiliyopo Mlandizi wilayani Kibaha yanayotarajiwa kuanza wakati wowote ili kujiimarisha kikakamavu na kujenga uzalendo wa nchi yao.
Aliyasema hayo hivi karibuni aliopoongea na waandishi wa habari mjini Kibaha na kusema kuwa mafunzo ya JKT ni muhimu hasa ikizingatiwa yanamfanya mshiriki kujua uzalendo wa nchi yake kama wanavyotarajia kwenda baadhi ya wabunge mafunzo hayo yatakapoanza.
Koka alisema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa watu wa aina yote na si kwa baadhi ya watu kwani waandishi wataweza kuielezea vizuri nchi yao pale watakapokuwa wakiandika habari zao.
“Kazi ya uandishi ni sawa na ya jeshi hivyo endapo watapata mafunzo hayo yatawasaidia kwa kiasi kikubwa katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku ambapo wamekuwa wakikutana na changamoto kubwa,” alisema Koka.
Aidha alisema kuwa kwa kipindi hichi waandishi wamekuwa wakishambuliwa hivyo endapo watapata mafunzo hayo yatawasaidia kujilinda na baadhi ya watu ambao wamekuwa wakiwateka waandishi na kuwadhuru.
“Zamani watu wengi walipitia mafunzo hayo kwa mujibu wa sheria hivyo kwa sasa kwa kuwa serikali imerejesha mafunzo hayo na waandishi nao wajitokeze ili waweze kupata mafunzo ambayo ni mazuri katika kuuweka mwili vizuri pia kuweza kujilinda,” alisema Koka.
Alibainisha kuwa waandishi kama baadhi ya wabunge waliojitokeza kushiriki mafunzo hayo nao wajitokeze, hivi karibuni serikali ilirudisha utaratibu wa mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria kuanzia mwaka huu.
Katika hatua nyingine alilaani baadhi ya watu ambao wamekuwa wakiwashambulia waandishi na kusema kuwa kufanya hivyo ni kunyanganya uhuru wa vyombo vya habari katika kufanya kazi zao.
Alisema inashangaza kuona waandishi wanashambuliwa pasipokuwa na sababu za msingi na kuwasababisha kufanya kazi zao kwa woga kuhofiwa kupigwa.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC-CCM) kutoka wilaya ya Kibaha mkoani Pwani Rugemalila Rutatina amewataka vijana kwenye wilaya hiyo kukitumia chuo cha ufundi Stadi (VETA) kilichopo wilayani humo ili kujiongezea ujuzi kuliko kuwaachia vijana kutoka mikoa mingine kusoma kwenye chuo hicho.
Aliyasema hayo hivi karibuni mjini Kibaha alipokutana na baadhi ya vijana kutoka kata mbalimbali kwenye wilaya ya Kibaha, kuzungumzia masuala ya kuboresha mazingira katika wilaya hiyo na kusema kuwa vijana wengi hawakitumii chuo hicho ambacho kimejengwa eneo la Kongowe.
Rutatina alisema kuwa inashangaza kuona vijana kwenye wilaya na mkoa wa Pwani kutokitumia chuo hicho licha ya wao kuwa jirani na chuo hicho huku vijana wengi kutoka mikoa mbalimbali nchini wakiwa wanakitumia ipasavyo chuo hicho.
“Changamoto kubwa inaonekana ni vijana wengi kutokukitambua chuo hicho kutokana na kukosa taarifa za uwepo wake jambo ambalo linawafanya washindwe kujiunga nacho hivyo vijana wanapaswa kutafuta taarifa na si kusubiri vijana toka nje ya mkoa wajae na kuanza kulalamika,” alisema Rutatina.
Alisema kuwa hiyo ni fursa ambayo vijana wa Kibaha na mkoa wanapaswa kuitumia kwani hata kama hawajafanikiwa kusoma masomo ya sekondari wana nafasi ya kujiunga na chuo hicho ambacho kinawapatia stadi za ufundi mbalimbali.
“Kama tujuavyo ufundi ni muhimu kwani kila kitu kinauhusiano na ufundi hivyo taaluma ya ufundi haiwezi kuepukika kwa maendeleo ya jambo lolote na hiyo ndiyo itakayowasaidia vijana katika mkoa wa Pwani kujikwamua na hali ngumu ya kiuchumi,” alisema Rutatina.
Aidha alisema kwamba hata masuala ya biashara na ujasiriamali yanafundishwa ambapo vijana wengi kwa sasa wamejiajiri na endapo watapata mafunzo ya chuo hicho wataweza kupata ujuzi na kuboresha shughuli zao.
“Maisha mazuri hayawezi kuja bila ya kujishughulisha kwani wakijiunga na mafunzo ya VETA wataweza kujiajiri na kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana kwani wataweza kujiajiri kupitia elimu watakayokuwa wameipata kwenye chuo hicho,” alisema Rutatina. Chuo hicho kilizinduliwa mwaka jana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Mwisho. 

Na John Gagarini, Kibaha
WAKAZI zaidi ya 1,500 wa Mtaa wa Zogowale, Kibaha Mjini mkoani Pwani, wanatarajia kunufaika na mradi wa maji ambao una uwezo wa kutoa maji lita 6,000 kwa saa.

Akizungumzia mradi huo wakati wa uzinduzi wa mradi huo ,mhandisi wa maji katika halmashauri ya mji wa Kibaha Grace Lyimo alisema idadi hiyo ya watakaonufaika ni sawa na asilimia 1.4 ya wananchi wa Kibaha Mjini hivyo kufanya jumla ya wanaopata maji kuwa ni asilimia 64.

Lyimo  alisema kuwa  ujenzi wa miundombinu ya mradi ulianza rasmi Mei 2012 na kukamilika mwaka huu kwa gharama ya zaidi ya shilingi Milioni 192 ambapo mkandarasi ameshakabidhiwa zaidi ya milioni 156 hadi sasa.

“Mradi  wa maji Zogowale uliibuliwa na jamii yenyewe na
wananchi walipaswa kuchangia zaidi ya milioni Nne ikiwa ni asilimia
2.5 ya gharama ya ujenzi ambapo waliweza kuchangia milioni moja na
laki saba na arobaini na tano, miasaba sabini na tano,” alisema Lyimo.

Aidha alisema kwa sasa mkandarasi anaendelea na umaliziaji wa kazi
ndogondogo zinazojitokeza na mfumo wa maji upo kwenye uangalizi kwa miezi sita.
Aliwataka wananchi kulinda miundombinu hiyo ya maji ili huduma hiyo iwe ya uhakika kwa lengo la kuondokana na kero ya maji katika mtaa huo.
Mwisho

No comments:

Post a Comment