Monday, March 25, 2013

WAIPONGEZA STARS


Na John Gagarini, Kibaha
WADAU wa soka mkoani Pwani wameipongeza timu ya Taifa kwa kuifunga Moroco kwa magoli 3-1 kwenye mchezo wa kufuzu kushiriki kombe la Dunuia nchini Brazil 2014 uliofanyika juzi kwenye uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na gazeti hili mjinin Kibaha moja ya wadau wa soka mkoani Pwani ambaye ni Mjumbe wa halmashauri Kuu ya Taifa Kibaha Mjini, Rugemalila Rutatina alisema kuwa timu hiyo imeonyesha kiwango kizuri kwa kuweza kukiangusha kigogo cha soka Barani Afrika.
Rutatina alisema kuwa Stars walionyesha mchezo mzuri ambao uliwavutia watu waliokwenda kuutazama na kusema sasa matumaini yameanza kuonekana kwenye soka la Tanzania.
“Tunawapongeza Vijana kwa kuonyesha kuwa wanaweza kwani waitoa Tanzania kimasomaso kwa kuwapa raha Watanzania kwa kuifunga Moroco ambao miaka ya nyuma walikuwa ni moja ya timu vigogo barani Afrika kutokana na uwezo wake kisoka,” alisema Rutatina.
Alisema kuwa miaka ya nyuma Watanzania walikuwa wakisikitishwa na matokeo yaliyokuwa yakitokea uwanjani kutokana na timu kufungwa mbele ya mashabiki wake lakini sasa wameweza kuibuka kidedea.
“Kwa kweli vijana wameitoa nchi kimasomaso na hichi ndicho Watanzania walichokuwa wakikitaka kwa miaka mingi tunawaomba wasibweteke na ushindi huu bali waongeze jitihada kwa kujituma zaidi kwenye michezo ijayo ili kwa mara ya kwanza Tanzania iweze kuingia kwenye ramani ya soka kwa kuingia kwenye kombe la dunia,” alisema Rutatina.
Aidha alisema kuwa jukumu lililobaki kwa shirikisho la soka nchini (TFF) ni kuitafutia Stars michezo mingi ya kirafiki hasa nje ya nchi ili kuwpaa uzoefu wachezaji hasa wale ambao bado hawajawa na uzoefu kwa michuano ya kimataifa.
“Stars itakuwa na michezo mingine ya nje hivyo lazima wachezaji wapate uzoefu mkubwa kama tunavyojua michezo ya ugenini huwa ni migumu kutokana na timu husika kutumia mazingira ya nyumbani kushinda,” alisema Rutatina.
Aliwataka wachezaji wa Stars kulinda viwnago vyao ili visishuke na kusababisha timu kufanya vibaya kwani bado kuna michezo migumu mbele yao ili kufuzu kucheza kombe la dunia.
Mwisho. 

 Na John Gagarini, Kibaha
BONDIA chipukizi Zumba Kukwe kutoka wilayani Kibaha mkoani Pwani anatarajiwa kupanda ulingoni dhidi ya Joseph Mbowe wa Jijini Dar es Salaam Aprili 7 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini kibaha bondia huyo maarufu kama Chenchidola alisema kuwa pambano hilo litafanyika kwenye ukumbi wa CCM Mwinjuma Mwananyamala Jijini Dar es Salaam.
Chenchidola alisema kuwa pambano lao hilo litakuwa ni la utangulizi kabla ya pambano la kugombea ubingwa kati ya Shaban Madilu na Issa Omary.
“Mchezo huo utakuwa ni wa kujiweka sawa kwani malengo ni kucheza kwenye mashindano mbalimbali lakini kwa sasa nafanya mapambano ya kujipima nguvu ili kujiimarisha kabla ya kukutana kuwania ubingwa,” alisema Chenchidola.
Alisema kuwa kwa sasa yuko imara kupambana na bondia yoyote hapa nchini lakini kabla ya kufikia kupambana na mabingwa lazima ajiweke sawa.
“Natarajia kumpiga kwenye raundi ya pili au ya tatu na si zaidi ya hapo hivyo akae sawa kwani nimejiandaa vilivyo katika mchezo huo na endapo atanipiga basi itabidi niombe pambano la marudiano,” alisema Chenchidola.
Aidha alisema kuwa lengo lake ni kupigana kwenye mapambano ya ubingwa ambapo kwa sasa anatarajia kupambana na bondia mkubwa hapa nchini ili awaonyeshe Watanzania kuwa anaweza.
Aliwataka mapromota kujitokeza kuwasaidia chipukizi ili nao waweze kufikia kwenye viwango vya juu kwani wengi wako hasa mikoani lakini hawapati nafasi.
Mwisho.    

   
   

No comments:

Post a Comment