Saturday, March 30, 2013

WALIMU WA RIADHA KUPEWA MAFUNZO


Na John Gagarini, Kibaha
IDARA ya Elimu na chama cha Riadha mkoa wa Pwani (RP) vimeandaa mafunzo kwa walimu wa mchezo wa riadha kutoka mikoa 10 kuanzia Aprili 6 hadi 17 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha mkufunzi wa chama cha Riadha Tanzania (RT) Robert Kalyahe alisema kuwa mafunzo yatakuwa ya siku 10 na yatafanyika kwenye uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha –Tumbi.
Kalyahe alisema kuwa mafunzo hayo ya hatua ya kwanza yatasimamiwa na RT ambapo vyeti vya wahitimu vitatambuliwa na chama cha Riadha Duniani (IAAF).
“Washiriki watakuwa kutoka mikoa 10 walengwa zaidi wakiwa ni walimu wa shule za msingi, sekondari na wadau wengine wa mchezo huo sifa ikiwa ni elimu ya kidato cha nne na kuendelea,” alisema Kalyahe.
Alisema kuwa RT imeamua kushirikisha walimu zaidi kwani wao wana nafasi kubwa kuwaandaa wanafunzi shuleni na wakufunzi watakuwa ni Seleman Nyumbani, Samwel Tupa na yeye mwenyewe.
Kalyahe ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya ufundi ya mkoa wa Pwani alisema kuwa hadi sasa ni wadau 26 wamejitokeza kushiriki mafunzo hayo na kuwataka wadau wengi zaidi kujitokeza kupata elimu hiyo ili waweze kuendeleza mchezo huo.
Mwisho.
    

No comments:

Post a Comment