WAAFANYAKAZI na Wazabuni mbalimbali wa Shirika la Elimu
Kibaha (KEC) mkoani Pwani wanalidai shirika hilo kiasi cha zaidi ya shilingi
biloni moja.
Hayo yalisemwa juzi na mkurugenzi wa shirika hilo Dkt Cyprian
Mpemba, wakati wa ziara ya siku moja ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Hawa Ghasia.
Dkt Mpemba alisema kuwa madeni hayo ni ya wazabuni wanaodai
kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 286, wafanyakazi wanaodai zaidi ya shilingi
milioni 277 na makandarasi mshauri wa hospitali ya Tumbi anayedai kiasi cha
zaidi ya shilingi milioni 600.
“Madeni hayo ni changamoto kwetu kwani ruzuku inayotolewa na
serikali haitoshelezi kabisa ambapo kwa bajeti ya mwaka 2010/2011 fedha
zilizotolewa na serikali zilikuwa ni pungufu kwa asilimia 15 huku bajeti ya
mwaka 2011/2012 ilikuwa pungufu kwa asilimia 48,” alisema Dkt Mpemba.
Alisema mbali ya madeni hayo pia shirika lina mahitaji
makubwa ambapo wanahitaji kiasi cha shilingi bilioni 11 kwa ajili ya kumalizia jengo
la hospitali, zaidi ya bilioni moja, milioni 500 kwa ajili ya mafunzo kwa
madaktari bingwa na wasaidizi, uchakavu wa majengo kiasi cha shilingi milioni
300, matengenezo ya magari na majengo zaidi ya milioni 131, maji, umeme, bima,
madawa na shajala shilingi zaidi ya milioni 143, chumba cha kuhifadhia maiti
shilingi milioni 160 kwa ajili ya ukarabati.
“Kutokana na changamoto ya fedha ripoti ya mkaguzi mkuu wa
serikali ya mwaka huu imetahadharisha kuwa shirika lipo kwenye hatari ya
kushindwa kabisa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwani inaonekana mahesabu
ya shirika yana mwelekeo mkubwa wa uhaba wa kumudu kulipa watoa huduma wastani
wa bilioni moja,” alisema Dkt Mpemba
Aidha alisema wastani wa mapato ya ndani ya shirika hilo ni
kati ya shilingi milioni 800 na bilioni moja kwa mwaka ambazo hazikidhi
matumizi stahiki kwa idadi ya watumishi waliopo 985 hivyo kuiomba serikali
kuongeza ruzuku ya mwaka kutoka bilioni 1.9 na kufikia bilioni 3.6.
Akijibu hoja hizo Waziri Ghasia alisema kuwa kuhusu madeni
watalifanyia kazi suala hilo ili kuweza kupunguza chanagamoto ya ukosefu wa
fedha kwenye shirika hilo la Umma ambalo limekuwa na mchango mkubwa ambayo ni
kutoa huduma za kielimu, afya na kupambana na umaskini.
‘Pia ifike wakati
mwende kwenye taasisi za kifedha kwa ajili ya kukopa kuliko kutegemea ruzuku ya
serikali ambapo kwa bajeti iliyopita hali ya kifedha haikuwa nzuri, kwani
mashirika ya umma yanatakiwa yajiendeshe yenyewe na si kuisubiri serikali pekee,”
alisema Ghasia.
Alisema KEC ina vyanzo vingi vya mapato ikiwemo ufugaji kuku
na ng’ombe endapo vitapatiwa fedha litaweza kujiendesha kwa kiasi fulani hivyo
kumudu kufanya shughuli zake za kila siku, awali Waziri alitembelea mashamba ya
kuku, kiwanda cha kutengenezea trei za mayai na hospitali ya Tumbi akiwa na
uongozi wa shirika na bodi.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment