Na John Gagarini,
Bagamoyo
MWALIMU wa shule ya
Msingi Msoga wilayani Bagamoyo mkoani Pwani anatuhumiwa kuwajaza mimba wanafunzi
wa shule ya msingi na mwingine wa sekondari Msoga huku mwingne akifumaniwa na
mwanafunzi.
Tuhuma hizo
zilibainika wakati wa kikao cha pamoja kati ya wazee maarufu viongozi wa dini,
wajumbe wa serikali ya Kijiji na watendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo
na mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Ahmed Kipozi.
Mwalimu huyo
alibainishwa kwenye kikao hicho ni Joel Mjema ambapo mwalimu mwingine ni Samwel
Mjema yeye anatuhumiwa kufumaniwa na mwanafunzi wa sekondari ya Msoga lakini
wazazi wa mwanafunzi huyo walilimaliza suala hilo kimya kimya.
Kutokana na tuhuma
hizo ambazo zinawakabili walimu hao mkuu wa wilaya hiyo Kipozi alitaka walimu
hao wakamatwe na kupelekwa kwenye vyombo vya kisheria ili hatua ziweze
kuchukuliwa kutokana na matukio hayo.
Akizungumzia tuhuma
za walimu hao Kipozi alisema kuwa mwalimu Joel Mjema ana tuhuma za
kumjaza mimba aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la sita katika shule hiyo jina
tunalo (Tatu Shaabani) hali iliyopelekea mwanafunzi huyo kushindwa kuendelea na
masomo yake ya kuhitimu elimu ya msingi.
“Lakini kwa kuona
hiyo haitoshi mwalimu huyo huyo akamjaza mimba na kupelekea kumkatisha
masomo mwanafunzi mwingine wa kidato cha tatu wa shule ya sekondari Lugoba na
Latifa Shaaban,na kuamua kuishi naye kinyumba kitu ambacho ni kibaya sana kwa
mwalimu aliyekabidhiwa dhima ya kulea watoto kimaadili,” alisema Kipozi.
Kuhusiana na
mwalimu Samwel Mjema alisema mwalimu
huyo anatuhumiwa kutembea na mwanafunzi (Maimuna Hamis) ambapo alifumaniwa na
wazazi wa binti huyo na kitu cha kushangaza suala hio lilimalizwa kimya kimya
baina ya mwalimu huyo na wazazi na binti hali aliyosema haikubaliki na
kuagiza mara moja kuchukuliwa hatua kwa wazazi wote ambao wamekuwa wakifikia
makubaliano ya kuvunja sheria.
Kipozi alisema kuwa
walimu hao kwa nyakati tofauti wamekuwa wakikiuka maadili na kanuni za utumishi
kwa kufanya ngono na wanafunzi wao kitu ambacho ni kinyume na kanuni na
taratibu za utumishi na sheria za nchi.
“Kwa ujumla
hatuwezi kuvumilia uchafu huu wa mtu anayepaswa kuheshimiwa kama mwalimu kuamua
kuanza kuwashawishi na kufanya ngono na wanafunzi wake lakini mbaya zaidi ni
kuwakatishia masomo watoto hao hivyo naagiza mara moja kukamatwa kwa walimu hao
na kufikishwa katika mikono ya sheria,” alisema Kipozi.
Hata hivyo taarifa
zilizotufikia zinasema kuwa mwalimu Samwel Mjema alikamatwa kuhusiana na tukio
lake na kutarajiwa kufikishwa mahakamani huku mwalimu Joel Mjema akitoroka
kuhusiana na tuhuma hizo zinazomkabili.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment