Na John Gagarini
MKUU wa mkoa wa Pwani Mwantumu
Mahiza amesema kuwa serikali haitakaa kimya kuona baadhi ya kinamama wakifanya
vitendo vya kinyama ikiwa ni pamoja na kutupa watoto wanaowazaa.
Mahiza aliyasema hayo wakati wa hafla fupi ya kusherehekea
siku ya Wanawake Duniani kwenye Halmashauri ya Mji wa Kibaha na kusema kuwa
baadhi wanawake wamekuwa wakiwafanyia ukatili hata watoto wao wa kuwazaa.
Alisema kuwa moja ya ukatili ambao umekithiri mkoani Pwani ni
kuwatupa watoto jambo ambalo limekuwa likishika kasi siku hadi siku kwenye mkoa
huo.
“Serikali haitaweza kuvumilia kuona baadhi ya akinamama
wakitenda vitendo vya ukatili kwa watoto wao kwani nao wana haki ya kulelewa na
wana haki ya kupata matunzo pamoja na kuishi hivyo ni vema kila mtu akatimiza
wajibu wake kwani hiyo ni haki ya msingi ya mtoto,” alisema Mahiza.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa haipendezi kuona wanawake
wanakuwa mstari wa mbele kufanya vitendo vya ukatili kwa watoto wao.
“Kama unaona bado hujajianda kulea kwanini uzae kama wewe
ungefanyiwa hivyo sasa hivi ungekuwa wapi na mtu wa aina gani ni lazima
mjilinde na kuachana na vietendo hivyo kwani ni ukatili ambao hutaweza
kuvumiliwa na serikali na hatua kali zitachukuliwa kwa wanaofanya vitendo hivyo,”
alisema Mahiza.
Aidha alisema vitendo hivyo ni vibaya kwani mbali ya kuwaua
watoto pia ni kuwafanya wawe watoto wa mitaani na kuathirika kisaikolojia na kuwajengea mazingira mabaya ya kuishi.
Kwa upande wake mke wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Selina
Koka alisema kuwa aliamua kuwakusanya wanawake kwa pamoja ili kubadilishana
mawazo na kutafakari siku hiyo katika kutimiza majukumu yao kama mama.
Koka alisema kuwa siku hiyo ina maana kubwa kwa akinamama
katika kuihudumia jamii na Taifa ambalo linawategemea katika kujenga uchumi wa
nchi.
Mwisho.
WAANDISHI wa Habari wa Kanda ya Mashariki wametakiwa kutoa
elimu ya kutosha kwa Jamii inayowazunguka ili kuondokana na dhana juu ya chanjo
mbalimbali zinazotolewa na serikali kwa watoto kuwakinga na magonjwa
yanayosababisha vifo.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na kaimu katibu Tawala mkoa wa
Pwani Injinia Michael Mrema wakati akifungua mafunzo ya siku moja juu ya chanjo
mpya ya magonjwa ya Nimonia na Uti wa Mgongo ya Rotavirus kwa waandishi wa
Kanda ya Mashariki.
Injinia mrema alisema kuwa jamii imekuwa na dhana mbaya kuwa
baadhi ya chanjo zina athari kwa watoto hivyo kushindwa kuwapeleka kupata
chanjo.
“Waandishi ni watu wanaoaminiwa na jamii hivyo kwa kutumia
kalamu zenu mnaweza kutoa elimu juu ya umuhimu wa chanjo hizo kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ambao
wanakufa kutokana na maambukizi ya magonjwa mbalimbali,” alisema Injinia Mrema.
Alisema kuwa magonjwa kama hayo husababisha vifo kwa asilimia
80 hivyo lazima itumike nguvu ya ziada ya kutoa elimu ili jamii ione umuhimu wa
kuwapeleka watoto wao kupata chanjo kwa lengo la kupunguza vifo hivyo visivyo
vya lazima.
“Chanjo hii mpya inatoa kinga kwa asilimia 87 hadi 88 ambapo
nchi imejitahidi sana kwani imeweza kupunguza vifo toka 99 hadi 51 kwa watoto
1,000 kwa mwaka 2010,” alisema Injinia Mrema.
Aidha alisema kuwa chanjo hiyo ni salama na haina madhara
yoyote na endapo jamii itapata taarifa sahihi hawataweza kupotoshwa na
watawapeleka watoto wao kupata chanjo hiyo ambayo ni bure na haina gharama
zozote.
Kwa upande wake ofisa habari idara ya habari maelezo Veronica
Kazimoto alisema kuwa mafunzo hayo kwa waandishi wa habari yatasaidia kufikisha
ujumbe sahihi na haraka kwa walengwa hivyo wanaamini kuwa waandishi ni njia
sahihi ya kutoa elimu. Mafunzo hayo ya siku moja waliwahusisha waandishi toka
mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.
Mwisho.
WAKAZI wa Mji wa Kibaha waliojenga vibanda na nyumba kwenye
maeneo ya barabara wametakiwa kuvunja mara moja kabla serikali haijavunja ili
kupisha matengenezo ya barabara za kuingia kwenye mitaa ya mji huo.
Hayo yalisema na Injinia wa Halmashauri ya Mji huo Ezekiel
Kunyaranyara alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa tayari
watendaji kwenye mitaa hiyo walishapewa barua ya kuwajulisha walengwa.
Kunyaranyara alisema kuwa baadhi ya watu wamejenga vibanda
vya biashara na nyumba kwenye eneo la barabara za mitaani na kufanya barabara
hizo kushindwa kupitika hasa pale yanapotokea madhara mbalimbali yakiwemo ya
moto.
“Athari za watu kujenga kwenye maeneo zinakopita barabara ni
nyingi lakini mojawapo ni magari kushindwa kupita hata pale kunapotokea mfano
mgonjwa anatakiwa kuchukuliwa na gari na kupelekwa hospitali au moto unapotokea
gari la zimamoto linashindwa kupita hivyo kuleta athari kubwa,” alisema
Kunyaranyara.
Alisema walitoa maelekezo kwa watendaji wa mitaa yote kwenye
maeneo husika na walitoa miezi sita tangu mwaka jana hadi Machi mwaka huu
ambapo endapo hawatafanya hivyo wakati wowote watatekeleza kazi hiyo.
“Katika awamu hii tulitenga kiasi cha shilingi milioni 9 kwa
ajili ya kuchonga barabara zote za Mji wa Kibaha kwani lengo ni kuhakikisha mji
unakuwa na barabara ambazo zinapitika kwa mkipindi chote cha mwaka,” alisema
Injinia Kunyaranyara.
Alisema kuwa hivi karibuni halmashauri ilinunua greda lake
hivyo kuanza kukarabati barabara zote kwenye kata zote za halmashauri hiyo 11
zenye mitaa 53.
KUFUATIA kilio cha mkuu wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza
kuiomba ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)
kuisaidia kupata fedha kiasi cha shilingi miloni 160 kwa ajili ya kukarabati
mochwari ya Hospitali ya Rufaa ya Tumbi hatimaye kilio hicho kimesikika ambapo
ofisi hiyo imeahidi kutoa fedha hizo.
Akizungumza juzi mara baada ya kutembelea Shirika la Elimu
Kibaha (KEC) lililopo wilayani Kibaha mbele ya viongozi wa shirika hilo ambalo
linamiliki hospitali hiyo, Kaimu katibu mkuu TAMISEMI Alafayo Kidata alisema
watatoa fedha hizo ili kufanya ukarabati wa chumba hicho.
Kidata alisema kuwa chumba hicho ni muhimu hivyo Wizara
imeona kuna umuhimu wa kutoa fedha hizo ili kufanya ukarabati kwani haipendezi
kuona chumba hicho kikiwa kwenye hali mbaya ambapo marehemu wanahifadhiwa humo.
“CHumba cha maiti ni muhimu sana na kila mtu atapitia hapo
hivyo kiubinadamu lazima mazingirra yake lazima yawe mazuri kutokana na maombi
toka kwa viongozi wa shirika tumeona mahali hapa panahitaji kuangaliwa mapema
huku sehemu nyingine zikifanyiwa kazi,” alisema Kidata.
Aidha alisema kuwa kutokana na umuhimu wa hospitali hiyo
kupokea majeruhi wengi wa ajali pamoja na maiti zinazopokelewa hapo ni vema
ukarabati ukafanyika ili kuondoa hali mbaya iliyopo.
“Tunatarajia mwishoni mwa mwezi huu fedha zitatolewa ili
kuboresha chumba hicho ambacho kwa sasa ni kidogo na kinapokea marehemu wengi,”
alisema Kidata.
Alibainisha kuwa madeni mbalimbali ambayo yanafikia kiasic ha
shilingi bilioni moja watahakikisha yanalipwa hadi ili huduma ziendelee
kutolewa kwani kuna hatari ya baadhi ya watoa huduma kusitisha.
Awali akitoa taarifa ya shirika kwa kaimu katibu mkuu,
mkurugenzi wa KEC Dkt Cyprian Mpemba alisema kuwa chumba cha maiti kwa sasa
kinahifadhi miili miwili miwili kutokana na udogo wake jambo ambalo si zuri.
Dkt Mpemba alisema kuwa chumba hicho hakijafanyiwa
matengenezo tangu hospitali hiyo ilipoanzishwa miaka ya 70 na wafadhili wa nchi
za Nordic, pia linakabiliwa na madeni makubwa yanayofikia zaidi ya bilioni
moja.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment