Na Mwandishi Wetu, Dodoma
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limetakiwa kuweka kitengo maalumu kitakachoshughulika na kusikiliza kero za kijinsia ili kuweka usawa wa kijinsia katika shirika hilo.
Hayo yamesemwa Jijini hapa na Naibu Waziri wa Nishati,Stephen Byabato katika uzinduzi wa Programu ya Mpango wa Jinsia wa miaka minne(2023-2027)wa TANESCO kwa kusirikiana na Benki ya Dunia kupitia mradi wa umeme wa Tanzania hadi Zambia(Tanzania-Zambia Transmission Interconnector Project-TAZA).
Naibu Waziri Byabato amesema kuwa Shirika hilo limekuwa likishughulikia masuala ya jinsia kwa namna mbalimbali hivyo kwasasa ni wakati muafaka wa kuwa na kitengo kitakachokuwa na bajeti,uongozi wa kitengo chenye uelewa na uweledi wa kusikiliza kero za kijinsia mbalimbali zitakazojitokeza.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO,Maharage Chande amesema kuwa lengo la programu hiyo kuwa ni kutatua changamoto wanazokutana nazo wanafunzi wanawake katika maeneo yao ya kazi kwa lengo la kukuza ajira zao ili kuongeza idadi ya wanawake wanaoajiriwa.
Mkurugenzi Chande ametaja maeneo ya kimkakati yatakayopewa kipaumbele kuwa ni kuiboresha sera ya Shirika na kujenga uwezo ili sera iende sambamba na masuala ya kijinsia,kuwepo na taarifa sahihi zinazohusu masuala ya unyanyasaji wa kijinsia kwenye Taasisi,kuruhusu fursa ya ukuzaji wa taaluma kwa wafanyakazi wanawake hasa wanaofanyakazi kwenye miradi na kuwepo kwa nafasi ya mafunzo kwa vitengo kwa wafanyakazi wanawake waliopo kazini ili kuwajengea uwezo kuelekea kwenye ajira kamili.
Aidha kuhusu mradi wa kusafirisha umeme wa Tanzania hadi Zambia (TAZA),Chande ameeleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Nishati na TANESCO wanatekeleza ujenzi wa mradi wa upanuzi wa njia ya kusafirisha umeme mkubwa wa kilovoti 400 kutoka katika kituo cha kupokea,Kupoza na kusafirisha umeme mkubwa cha Tagamenda Iringa kwenda kwenye nchi zilizopo kusini mwa Tanzania(Southern African Power Pool)kupitia Kisada Iringa,Iganjo Mbeya na Nkangamo Tunduma Songwe.
Chande amekitaja kituo hicho cha Tagamenda kuwa ni kitovu cha kusafirisha umeme mkubwa wa kilovoti 220 kwenda kwenye mikoa takribani 18 nchini.
Na kwa upande mwingine kituo hiki kimeunganishwa na kituo cha umeme cha zuzu Dodoma ili kusafirisha umeme mkubwa kwenda kwenye nchi zilizopo Mashariki mwa Tanzania ambazo ni Kenya,Uganda na Ethiopia kupitia mradi wa kuunganisha umeme baina ya Kenya na Tanzania(Kenya-Tanzania Power Interconnection Project-KTPIP)
No comments:
Post a Comment