Wednesday, March 22, 2023

CHAVITA YAIPONGEZA eGA KWA HUDUMA ZA SERIKALI MTANDAO JUMUISHI KWA WATU WENYE ULEMAVU

 

MWENYEKITI  wa Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) Wilaya ya Rufiji Mkoa wa Pwani Suleiman Zalala ameipongeza Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kwa huduma jumuishi za utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao kwa watu wenye ulemavu.

Zalala ametoa pongezi hizo wakati wa kilele cha kikao kazi cha Serikali Mtandao kilichofanyika hivi karibuni katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa (AICC) Jijini Arusha.

Zalala ameishukuru Mamlaka kwa kuthamini na kuona mchango wa kundi maalumu la watu wenye ulemavu kushiriki katika mafunzo hayo ili kuboresha huduma jumuishi za Serikali Mtandao kwa watu wenye walemavu.

"CHAVITA imekuwa na ushirikiano wa muda mrefu na eGA katika mipango mbalimbali ya mafunzo inayoandaliwa na Mamlaka kwa watu wenye ulemavu na kwamba mafunzo hayo yamekuwa yakiwajengea uwezo na uelewa mkubwa wa utekelezaji wa jitahada za Serikali Mtandao katika utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi,"amesema Zalala.

Amesema kubwa wameweza kujifunza na kupata uelewa juu ya mabadiliko mbalimbali ya teknolojia katika utoaji wa huduma na huduma mbalimbali zinazowezeshwa na eGA kwa wananchi kama vile ununuzi wa Luku, kata za maji n.k

Aidha ameomba mafunzo hayo yawe chachu kwa Taasisi nyingine za Umma kuiga mfano wa kile kilichofanywa na Mamlaka kwa kuwashirikisha makundi maalum kwenye uandaaji wa mafunzo na mipango mbalimbali inayotekelezwa na taasisi zao .

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi Benedict Ndomba amewashukuru wadau wote waliohudhuria kikao kazi hicho na kwa michango yao itakayosaidia kufanikisha na kuimarisha utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao kwa ajili ya kuboresha utendaji kazi wa Taasisi za umma, pamoja na utoaji wa huduma kwa umma.

“Naimani kuwa kikao hiki kimewajengea uwezo zaidi washiriki wote kuhusu Serikali Mtandao na kila mdau ametambua namna ambavyo anaweza kufanikisha jitihada za Serikali Mtandao kupitia sekta yake,"amesema Mhandisi Ndomba

Mhandisi Ndomba ameongeza kuwa washiriki zaidi ya 1624 wamehudhuria kikao hicho na mada 22 ziliwasilishwa na wadau kutoka katika taasisi mbalimbali za Umma zilizolenga kutathmini na kuimarisha nguzo kuu Nne (4) za Serikali Mtandao.

Amesema kuwa katika kikao hicho wadau wamepata fursa ya kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano katika kutekeleza jitihada za Serikali Mtandao nchini pamoja na kutafuta ufumbuzi wa changamoto za serikali mtandao zilizopo nchini ili kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii .

Amebainisha kuwa washiriki wametoa maoni mbalimbali ya namna ya kukuza jitihada za Serikali Mtandao ikiwa ni pamoja na kushauri uboreshaji wa Mifumo mbalimbali inayotoa huduma kwa umma pamoja na kupanua wigo wa utoaji wa huduma za Serikali Mtandao katika maeneo mbalimbali nchini.


Mkurugenzi amesema Menejimenti ya Mamlaka imeyapokea maoni na ushauri uliotolewa na kwamba eGA ipo tayari kufanyia kazi maoni hayo yanayolenga kuboresha na kukuza jitihada za Serikali Mtandao nchini.

No comments:

Post a Comment