JESHI la Polisi Mkoani Pwani linawashikilia watu 67 kutokana na makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na tuhuma ya kukutwa na silaha moja aina ya gobore.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kamanda wa Polisi Mkoani Pwani (ACP) Pius Lutumo alisema kuwa watu hao walikamatwa kwenye misako na opereseheni zilizofanywa katika kipindi cha wiki mbili Machi Mosi hadi Machi 14.
Lutumo alisema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa kutokana na tuhuma za makosa mbalimbali ambapo watapelekwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
"Lengo la misako hiyo ni kuzuia uhalifu ambapo tunawashukuru wananchi kwa ushirikiano ili kufanikisha kukabiliana na uhalifu,"alisema Lutumo.
Alitaja baadhi ya vitu vingine vilivyokamatwa ni pamoja na bhangi viroba vitatu, puli 102 na kete 789 na pombe ya moshi lita 143 na mtambo mmoja wa kutengenezea pombe hiyo.
"Vitu vingine ni pikipiki 10 ambazo zina usajili wa aina tofauti isipokuwa pikipiki tatu ambazo hazina usajili na watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani mara upelelezi utakapokamilika,"alisema Lutumo.
Aidha alisema kuwa Polisi inatoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kuhusiana na taarifa za uhalifu na wahalifu ili kuendelea kuufanya mkoa kuwa shwari.
No comments:
Post a Comment