Friday, March 31, 2023

MAHAKIMU NA MAJAJI WAPATIWA MAFUNZO

 

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

MAHAKIMU na Majaji wamepatiwa mafunzo ya siku mbili kuhusu wajibu wa Mahakama katika kutunza na kulinda uhuru wa kujieleza pamoja na haki za binadamu nchini.

Mafunzo hayo ya siku mbili yanatolewa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) likiwa Ni kukumbushana masuala mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Mratibu wa Mtadao wa THRDC, Onesmo Olengurumwa akizungumza na waandishi wa habari  jijini dodoma wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo kwa Mahakimu na Majaji nchini amesema lengo ni kukumbushana wajibu katika kutekeleza majukumu ya kila siku.

Aidha amesema kuwa umekuwepo na mabadiliko mengi ya kisheria na masuala mbalimbali yanayohusu haki za binadamu hivyo wao kama watu ambao wanatoa haki kila siku katika Mahakama, wanapaswa kuyafahamu ili kulinda haki za binadamu na uhuru wa kujieleza

Amesema pia mafunzo mengine ambayo yatatolewa ni masuala ya maadili kwa Mahakimu na Majaji katika utekelezaji wa majukumu ya utoaji wa haki katika maeneo yao.

Amesema Suala la maadili ni jambo la muhimu sana katika mahakama zetu nchini hivyo mafunzo haya pia yatasaidia kuwakumbusha Mahakimu na Majaji wajibu wao wa kutenda haki kwa kuzingatia maadili ya kazi zao.

Naye Naibu katibu mkuu wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (JMAT) Mary Kallomo, amesema mafunzo hayo yatawasaidia kuboresha utendaji wao wa kila siku katika kulinda haki za binadamu na uhuru wa kujieleza.

No comments:

Post a Comment