Thursday, March 2, 2023

WATAKA KUHARAKISHWA UJENZI NYUMBA YA MKURUGENZI NA WAKUU WA IDARA

MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha wametaka kuharakishwa ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi na wakuu wa Idara kwani imepita muda mrefu ujenzi huo bado haujaanza.

Wakizungumza kwenye kikao cha baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo walisema kuwa kwa kuwa tayari azimio la ujenzi huo limeshapitishwa hakuna sababu ya kuchelewesha ujenzi.

Diwani wa Kata ya Mtambani Godfrey Mwafulilwa alisema kuwa kama hakuna changamoto yoyote ni vema kuanza ujenzi ili watumishi hao wawe na makazi ndani ya Halmashauri.

Mwafulilwa alisema kuwa kama eneo hilo halina mgogoro wowote kwanini ujenzi hauanzi ambapo eneo hilo ni jirani na ilipojengwa hospitali ya Wilaya.

"Tunataka kikao kijacho tupate majibu kuwa ujenzi unaanza lini ili tuweze kuufanya kwa wakati kwani hakuna sababu ya kuchelewesha ujenzi,"alisema Mwafulilwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Erasto Makala alisema kuwa baadhi ya Madiwani walikuwa na hofu kuwa eneo hilo lilikuwa na migogoro.

Makala alisema kuwa eneo hilo lilikuwa na migogoro baadhi ya watu waliibuka na kusema ni lao hivyo kama lina changamoto ni vema wakaelezea ili waweze kujua.

Naye Ofisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Brown Nziku alisema kuwa eneo hilo zamani lilikuwa likimilikiwa na Taasisi ya Mkonge na kupewa kampuni ya UFC lakini ilifutiwa hati na Rais ambapo watu walilivamia.

Nziku alisema kuwa baada ya kurudishwa serikalini ilikabidhiwa Halmashauri ambapo walipewa hekari 9.5 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi na wakuu wa Idara.

Alisema kuwa kwa sasa hatua iliyofikiwa ni ya manunuzi na baada ya hapo ujenzi utaanza mara moja.


No comments:

Post a Comment