Tuesday, March 7, 2023

OSHA YAPATA MAFANIKIO

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WAKALA wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) imefanikiwa kuongeza idadi ya maeneo ya kazi yaliyosajiliwa kutoka 4,336 hadi 11,953.

Aidha ongezeko hilo ni sawa na asimilia 276 na  idadi ya kaguzi zilizofanyika zimeongezeka kutoka kaguzi 104,203 hadi kufikia kaguzi 322,241 sawa na asilimia 132.

Hayo yameelezwa na Mtendaji Mkuu wa OSHA  Khadija Mwenda akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali na utekelezaji wa majukumu ya Wakala hiyo Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Mwenda amesema kuwa kumekuwa na ongezeko la upimaji afya za wafanyakazi kwa asilimia 320 upimaji wa afya kutoka wafanyakazi 363,820 hadi kufikia wafanyakazi milioni 1.1 waliopimwa katika kipindi hicho cha miaka miwili kutotokana na kupunguzwa kwa ada mbalimbali.

Amesema kuwa kuboreshwa mifumo ya usimamizi ambayo imewezesha maeneo mengi ya kazi kukaguliwa wafanyakazi wengi kupimwa afya na mafunzo mbalimbali kufanyika ongezeko hilo ni tafsiri kwamba hali ya usalama na afya  katika maeneo ya kazi inazidi kuimarika.

Ameongeza kuwa ongezeko la asilimia 175 ya wafanyakazi waliopata mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi kutoka wafanyakazi 32,670 hadi kufikia wafanyakazi 43,318. 

"Katika kusimamia Sheria ya Usalama na Afya kwa lengo la kuzuia ajali magonjwa na vifo vitokanavyo na kazi maeneo ya kazi ambayo hayakuzingatia Sheria na Kanuni za Usalama na Afya yalichukuliwa hatua mbali mbali za kisheria zikiwemo kupewa hati ya maboresho (Improvement Notice) ambapo maeneo ya kazi 1,588 yalipewa hati hizo na maeneo ya kazi mengine 105 yalitozwa faini,"amesema Mwenda. 

Amebainisha kuwa miongoni mwa majukumu ya OSHA ni kuchunguza ajali mbali mbali zinazotokea katika sehemu za kazi kwa lengo la kubaini vyanzo vya ajali hizo ili kushauri namna bora ya kuzuia ajali kutokea tena.

Dhima kuu ya  Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) ni kuelimisha na kuhamasisha masuala ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi kwa kuweka mifumo thabiti itakayo zuia ajali, magonjwa na vifo pamoja na uharibifu wa mali ili kupunguza gharama za uendeshaji na kukuza uchumi wa Taifa.


No comments:

Post a Comment