WATU nane wamejeruhiwa baada ya basi walilokuwa wakisafiria la kampuni ya Happy Nation kutoka Bukoba kwenda Dar es Salaam kuacha njia na kupinduka.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kamanda wa Polisi Mkoani Pwani ACP Pius Lutumo alisema kuwa basi hilo lilipinduka baada ya kujaribu kulipita gari lililokuwa limesimama.
Lutumo alisema kuwa ajali hiyo ilitokea Februari 2 mwaka huu majira ya 8:30 usiku kwenye Kijiji cha Ruvu Kata ya Vigwaza Wilaya ya Kipolisi Chalinze Bagamoyo.
"Basi hilo lenye namba za usajili T 526 DVJ lilikuwa likiendeshwa na Vincent Mbasha (39) mkazi wa Mbezi Jijini Dar es Salaam na chanzo lilikuwa likilikwepa gari la mizigo aina ya Scania lenye namba T 299 BYF na tela namba T 308 BYF lilikuwa limepata hitilafu na kutoweka alama yoyote kuashiria kuwa kuna gari ndipo dereva huyo wa basi akalikwepa na kupinduka,"alisema Lutumo.
Alisema kuwa basi hilo lilikuwa na abiri 47 ambapo majeruhi wako hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi kwa matibabu zaidi ambapo hali zao zinaendelea vizuri.
Aidha aliwataja majeruhi hao kuwa ni Nuru Mohamed (38), Selimanda Abdala (63), Amina Jumanne (48), Faudhia Ismail (23), Fredina Omary (15) Abtatus Jovin (18), Idat Reman (27) na Aida Suleiman (24).
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ambaye aliwatembelea majeruhi hao alisema kuwa madereva wanapaswa kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zisizo za lazima.
Kunenge alisema kuwa alipata taarifa kuwa dereva huyo alitaka kulipita gari hilo upande wa kulia badala ya kushoto ambapo ni uzembe hivyo ni vema wakazingatia sheria.
Naye Mganga mfawidhi wa Tumbi Amani Malima alisema kuwa waliwapokea majeruhi hao ambapo wameumia maeneo mbalimbali ya miili yao na wanaendelea vizuri na matibabu.
Malima alisema kuwa wagonjwa hao wanaendelea na vipimo mbalimbali vikubwa ilikugundua majeruhi hao wameumia kiasi gani.
No comments:
Post a Comment